Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Josephine Kapoma, amewahimiza wajasiriamali wadogo, hususan wanawake, kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ili kujiimarisha kiuchumi na kuongeza kipato chao.
Kapoma alitoa wito huo alipowatembelea wajasiriamali katika Kata za Kingo na Bigwa, Manispaa ya Morogoro, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Katika ziara hiyo, amepata fursa ya kuzungumza na vikundi vya wanawake wanaojishughulisha na biashara ndogondogo, upishi wa vyakula (maarufu kama mama lishe), pamoja na shughuli nyingine za kujiongezea kipato.
Akizungumza na wajasiriamali hao, Mbunge huyo amewahamasisha kutumia kikamilifu mikopo inayotolewa kupitia halmashauri, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotengwa kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Akieleza kuwa fursa hizo zimeanzishwa mahsusi kuwawezesha wananchi wa makundi hayo kiuchumi na kuwapa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Kapoma amesisitiza kuwa ni wakati muafaka kwa wanawake kuondoa hofu na kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo pamoja na kushiriki katika mafunzo ya ujasiriamali yanayoratibiwa na Serikali na taasisi mbalimbali. Alibainisha kuwa nidhamu katika matumizi ya mikopo, uwajibikaji na mshikamano ndani ya vikundi ni mambo muhimu yatakayosaidia kuhakikisha wanufaika wanapata matokeo chanya na kurejesha mikopo kwa wakati.
Aidha, Mbunge huyo ameeleza kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa mwanamke katika jamii, akisisitiza kuwa wanawake ni walezi, wahimili wa familia na nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa. Ameongeza kuwa uwekezaji kwa mwanamke ni uwekezaji kwa jamii nzima, kwani mwanamke anapowezeshwa kiuchumi huimarisha ustawi wa familia na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Kapoma pia ametoa mitaji kwa baadhi ya vikundi vya wajasiriamali aliowatembelea, hatua inayolenga kuwawezesha kupanua biashara zao na kuongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi.
Kwa upande wao, baadhi ya wajasiriamali waliopata fursa ya kuzungumza walimshukuru Mbunge huyo kwa kuwafikia na kusikiliza changamoto zao. Wameeleza kuwa mafunzo na mikopo ya riba nafuu vitasaidia kukuza biashara zao, kuongeza kipato na kuboresha maisha yao pamoja na familia zao.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika shughuli za maendeleo na kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa vitendo, kwa kuweka mkazo katika uwezeshaji wa kiuchumi na usawa wa kijinsia.
