Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. Deodatus Mwanyika, ameeleza kuridhishwa kwake na hatua ya ujenzi wa jengo la kisasa la Vipimo na Viwango katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Machi 12, 2026, Mhe. Mwanyika amebainisha kuwa mradi huo wa ghorofa 10 umefikia asilimia 93 ya utekelezaji wake, jambo linaloashiria usimamizi madhubuti na weledi katika ukamilishaji wa Jengo Jengo hilo ili kukidhi ongezeko la wanafunzi wanaodahiliwa kila mwaka.
Vilevile, Mwenyekiti huyo ametoa rai kwa uongozi wa chuo kuendelea kutoa na kuimarisha elimu ya kati (middle-level education) katika fani za biashara hususani ujasiliamali kwa kuwa ni nyenzo adhimu kwa wahitimu wanaojiandaa kuingia kwenye soko la ajira binafsi na Kutasaidia kuongeza hadhi ya chuo na kuchochea ari ya wanafunzi wengi zaidi kujiunga na taasisi hiyo.

Amesema kuwa uimara wa chuo unategemea ubora wa mafunzo unayoyatoa na uwezo wake wa kuzalisha wataalamu wenye ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, amefafanua kuwa mradi huo unatekelezwa kupitia bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2025/26 na unatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba zaidi ya wanafunzi 4,000 kwa wakati mmoja.
Aidha amebainisha kuwa Jengo hilo la Vipimo na Viwango litakuwa kitovu cha mafunzo ya masoko na nyanja mbalimbali za kibiashara ambazo zinahitajika kwa kiasi kikubwa kulingana na mwelekeo wa sasa wa uchumi wa viwanda.
Naye Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Prof. Edda Lwoga, ameeleza kuwa mradi huo ulioanza Mei 25, 2023, umekuwa mhimili wa mabadiliko makubwa ya kitaaluma chuoni hapo. Alibainisha kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza fursa za udahili kwa wanafunzi wengi wanaohitaji masomo ya biashara na ujasiriamali, ikiwemo kozi fupi ambazo zimekuwa na mahitaji makubwa kwa wadau wa sekta binafsi.
