Latest Posts

KAMISHNA MPYA WA UHIFADHI WA TANAPA AAPISHWA RASMI

📌 ATAKIWA KUJENGA NIDHAMU ISIYOTETEREKA KWA ASKARI NA KUJALI MASLAHI YAO.

Na, Mwandishi Wetu – ARUSHA

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amemuapisha Kamishna Massana Gibril Mwishawa kuwa Kamishna mpya wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na kumtaka kuimarisha mapambano dhidi ya ujangili na uhalifu wa wanyamapori, kwa kutumia teknolojia za kisasa na mifumo madhubuti ya kiintelijensia.

Akizungumza Jijini Arusha, katika hafla ya kumuapisha na kumvalisha cheo Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Dkt. Kijaji amesema, uteuzi huo ni ishara ya imani aliyonayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya Kamishna Mwishawa hususani kuhusu uzoefu, uzalendo, kujituma na utendaji mzuri na mchango katika sekta ya uhifadhi na utalii kwa Shirika na nchi kwa ujumla.

Ameongeza kuwa Serikali na Wizara ina matarajio makubwa kuwa Kamishna Mwishawa ataiongoza TANAPA kwa weledi, uadilifu, nidhamu, umoja na maono yatakayoiwezesha taasisi hiyo muhimu kwa uhifadhi na utalii nchini kuendelea kuwa mfano bora Nchini, Afrika na Duniani kwa ujumla.

“Ufanisi wa TANAPA katika kulinda bioanuai, kupambana na ujangili, kudhibiti uvamizi na kulinda rasilimali za taifa, unategemea kwa kiwango kikubwa uwepo wa askari na afisa wenye nidhamu, uadilifu, uzalendo na weledi wa hali ya juu sana.

Dkt. Kijaji amemuagiza Kamishna Mwishawa kuhakikisha anajenga nidhamu isiyotetereka kwa maafisa na askari wa shirika hilo, kwa kuhakikisha sheria, kanuni na maadili ya utumishi yanazingatiwa wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao na kwamba Serikali hatavumilia vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, ukatili usiozingatia sheria, utovu wa nidhamu, kutokuwajibika, matumizi mabaya ya mali za serikali, wala vitendo vyovyote vinavyochafua taswira ya TANAPA na serikali yetu kwa ujumla.

Amemtaka Kamishna huyo kuzingatia kwa mujibu wa sheria na taratibu za serikali maslahi ya watumishi na kuhakikisha muda wote maslahi ya watumishi yanapewa kipaumbele sambamba na kuboresha mazingira ya kazi ikiwa ni pamoja na kuongeza nyumba za watumishi na askari, vitendea kazi, kuimarisha mafunzo, huduma za afya.

“Hapa Kamishna wa Uhifadhi, naomba upigie mstari, ninatarajia kuona TANAPA ikiwa taasisi inayojivunia watumishi wenye maadili, nidhamu, ari ya kazi,na uzalendo wa hali ya juu. Jenga utamaduni wa kuthamini watumishi wanaofanya vizuri huku ukichukua hatua za haraka na za haki kwa wale watakaokiuka sheria, kanuni na maadili ya kazi zao,” alisisitiza Dkt. Kijaji.

Kwa upande wake Kamishna mpya wa Uhifadhi wa TANAPA, Missana Mwishawa amesema anatambua kuwa nafasi ya Kamishna wa Uhifadhi, si heshima pekee bali ni dhamana kubwa yenye wajibu wa kulinda moja ya urithi muhimu zaidi wa taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!