Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amekemea vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akisema vinaathiri ubora wa miradi, vinachelewesha utekelezaji wake na kusababisha baadhi ya miradi kukamilika chini ya viwango vinavyotarajiwa.

Malima amesema hayo Julai 10, 2026, wakati akifungua warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Morogoro iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Amesema rushwa haimaanishi kutoa au kupokea fedha pekee, bali inajumuisha vitendo vyote vinavyokiuka taratibu, sheria na maadili kwa lengo la kujipatia manufaa binafsi, hali inayowafanya baadhi ya watendaji kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na ufanisi.
Kutokana na hali hiyo, Malima ameitaka TAKUKURU kuendelea kusimamia kwa karibu watendaji na wataalamu wanaohusika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi, huduma bora zinawafikia wananchi na miradi yote inatekelezwa kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha.

Kwa upande wake, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Pilly Mwakasege, amesema rushwa ni miongoni mwa sababu zinazosababisha kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuongeza gharama zisizo za lazima na kusababisha miradi kutokidhi thamani ya fedha (value for money). Amesema warsha hiyo inalenga kuimarisha uwajibikaji na usimamizi wa miradi, sambamba na kaulimbiu isemayo, “Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu; tutimize wajibu wetu.”
