Latest Posts

MVUTANO MKALI RAIS KUITWA MAHAKAMANI, JAMHURI YAPINGA/ KESI ‘YASIMAMA’ KWA MUDA

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, imechukua sura mpya leo Agosti 21, 2026 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, baada ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru kumkuta na kesi ya kujibu. Uamuzi huo unamaanisha kuwa Lissu ataendelea kusota gerezani huku akitakiwa kuanza kujitetea kwa kuwaleta mashahidi wake mahakamani.

Baada ya kuelezwa haki zake, Lissu aliijulisha mahakama kuwa atajitetea mwenyewe kama shahidi wa kwanza na kuwasilisha orodha ya mashahidi wengine anaotaka waitwe kisheria (summons). Orodha hiyo ilijumuisha viongozi wakuu na wastaafu wa serikali pamoja na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, wakiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, Philip Isdor Mpango, Kassim Majaliwa Majaliwa, IGP Camilius Wambura, CDF Jenerali John Mkunda, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), na DCI CP Ramadhan Kingai. Aidha, aliorodhesha viongozi wa CHADEMA ambao ni John Mnyika, Amani Golugwa, John Heche, na Brenda Rupia.

Upande wa Jamhuri, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Nassor Katuga, ulipinga vikali mashahidi viongozi wakuu wa serikali na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama kuitwa mahakamani. Katuga alidai kuwa mashahidi hao hawakutajwa wakati wa mchakato wa awali wa ukabidhi (committal proceedings) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kwamba watumishi wa umma tayari walishatoa ushahidi kwa niaba ya Rais.

Lissu alijibu mapingamizi hayo kwa kueleza kuwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Kisutu, Franco Kiswaga, alikataa kurekodi majina ya mashahidi wake akimtaka akawataje Mahakama Kuu. Lissu alisisitiza kuwa viongozi hao wana ushahidi muhimu sana kwasababu shitaka linalomkabili linahusisha nia ya kuitishia serikali. Aliongeza kuwa hata viongozi wastaafu kama Mpango na Majaliwa hawana ulinzi wa kisheria unaozuia kuitwa mahakamani.

Baada ya kusikiliza mabishano hayo ya kisheria, jopo la majaji liliamua kuwa halina pingamizi kwa mashahidi wa nane hadi wa 11 (ambao ni viongozi wa CHADEMA: Mnyika, Golugwa, Heche, na wengineo) na kuamuru waendelee kutoa ushahidi. Kuhusu mashahidi wa serikalini waliowekewa pingamizi, majaji walieleza kuwa watatoa uamuzi wao katika tarehe itakayotajwa baadaye.

Kufuatia uamuzi huo, Lissu aliomba mahakama kutoa mapumziko mafupi ili aweze kushauriana na mashahidi hao wa CHADEMA walioruhusiwa, akieleza kuwa hajaonana nao tangu Novemba mwaka jana. Majaji waliridhia ombi hilo na kutoa mapumziko hadi saa tisa na nusu mchana, ambapo kesi hiyo imeamriwa kuendelea leo kwa kuwasikiliza mashahidi hao waliopo mahakamani ambao kiuhalisia ni viongozi waandamizi wa CHADEMA.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!