Latest Posts

MNYIKA AINGIA KIZIMBANI, ASEMA YEYE NDIYE ALIYEANDAA MKUTANO WA APRILI 3, SI LISSU

Shauri la uhaini namba 19605/2025 linalomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Antiphas Lissu, limechukua mwelekeo mpya Agosti 28, 2026, baada ya Shahidi wa Pili wa upande wa utetezi, John John Mnyika, kupanda kizimbani kutoa ushahidi ili kuisambaratisha kesi hiyo ya Jamhuri.

Kesi hiyo ilirejea tena mahakamani saa 8:38 mchana kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa mashahidi wa upande wa utetezi baada ya Tundu Lissu kumaliza kutoa ufafanuzi wake (Re-examination). Lissu alisimama mahakamani hapo na kumuongoza Mnyika, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa CHADEMA, kuanza kutoa ushahidi wake wa utetezi.

Katika utangulizi, Mnyika ameisaidia mahakama kuelewa wasifu na tajriba yake ndani ya CHADEMA na katika ulingo wa siasa za kitaifa. Alieleza kuwa ameshikilia nafasi ya ukatibu mkuu wa chama hicho tangu mwaka 2019. Kabla ya kushika wadhifa huo, alihudumu katika nafasi mbalimbali za uongozi tangu ujana wake ikiwamo Mkurugenzi wa Vijana CHADEMA Taifa, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa CHADEMA, na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa kichama Kinondoni.

Nje ya chama, Mnyika ameeleza kuwa alikuwa Mbunge wa Jimbo la Ubungo kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, na baadaye Mbunge wa Jimbo la Kibamba kuanzia mwaka 2015 hadi 2020. Katika kipindi chote hicho bungeni, alichaguliwa kuwa Katibu wa wabunge wote wa CHADEMA.

Mnyika amefafanua muundo wa kiutawala wa CHADEMA ili kubainisha nani anayehusika na uendeshaji wa shughuli za kila siku za chama. Ameeleza kuwa Katibu Mkuu ndiye Mtendaji Mkuu wa chama na ndiye Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Chama Taifa- chombo kinachohusika na utendaji na uendeshaji wa kila siku wa chama. Majukumu ya nafasi hiyo ni pamoja na kusimamia rasilimali, utawala, utekelezaji wa maamuzi ya vikao vya juu vya kikatiba (kama Baraza Kuu, Kamati Kuu, na Mkutano Mkuu), na kusimamia watumishi wa makao makuu ya chama.

Alipoulizwa na Lissu kuhusu utaratibu wa kuitisha mikutano ya ndani ya kikatiba na ile ya hadhara, Mnyika ameeleza kuwa maandalizi yote hufanywa na Sekretarieti ya chama taifa chini ya usimamizi wa Katibu Mkuu.

Wajumbe wa Sekretarieti hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu (kama Mwenyekiti), Manaibu Katibu Wakuu wawili (Bara na Zanzibar), wakurugenzi wa kurugenzi za chama, wataalamu, Katibu wa Sekretarieti, na makatibu wa mabaraza ya chama (BAZECHA, BAWACHA, na BAVICHA).

Mnyika ameweka msisitizo mkubwa kwa kueleza kuwa: “Mwenyekiti (Tundu Lissu) si sehemu ya Sekretarieti ya chama taifa na hashiriki hata kidogo katika mikutano hiyo au maandalizi yake ya kiutendaji.”

Shtaka la uhaini linalomkabili Lissu linadai kuwa mnamo tarehe 3 Aprili 2025, alitengeneza nia ya kuhamasisha umma kuvuruga uchaguzi mkuu kwa kuitisha mkutano wa watia nia. Mnyika amelieleza jopo la majaji kuwa ana ufahamu kamili wa mkutano huo wa tarehe 3 Aprili 2025 kwa sababu “uliandaliwa chini ya maelekezo yake mwenyewe na Sekretarieti anayoiongoza, ambapo yeye mwenyewe ndiye aliyegawa majukumu ya maandalizi ya mkutano huo.”

Mnyika alifichua kuwa wakati maandalizi yote ya mkutano huo yanafanyika, Tundu Lissu hakuwa Dar es Salaam bali alikuwa mkoani akiongoza ziara ya Kanda ya Nyasa (inayojumuisha Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, na Rukwa) kuanzia tarehe 23 Machi hadi tarehe 3 Aprili 2025 kuhamasisha kampeni ya “No Reforms No Election”. Lissu hakuhusika kwa namna yoyote ile katika maandalizi ya mkutano huo wala kualika watia nia au waandishi wa habari.

“Tuhuma hizi kwamba Mwenyekiti Lissu ndiye aliyeandaa mkutano na kualika waandishi wa habari ni tuhuma za uongo na za kubambikiza kabisa,” amesema Mnyika kwa msisitizo mbele ya majaji.

Kuhusu uwepo wa waandishi wa habari na zana zao za kazi (kama kamera za Sony NX zilizotajwa na Jamhuri), Mnyika ameeleza kuwa waandishi wa habari walialikwa kwa ujumla kupitia Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chama, Brenda Rupia, kufuatia taarifa ya umma iliyotolewa tarehe 27 Machi 2025. Amesisitiza kuwa chama hakikutoa maelekezo yoyote kwa waandishi wa habari kuhusu vifaa wanavyopaswa kuja navyo au jinsi ya kurusha matangazo hayo, kwani CHADEMA inaamini katika uhuru wa vyombo vya habari.

Aidha, amesema kuwa kikao kiliendeshwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilishirikisha waandishi wa habari kuchukua hotuba za viongozi (akiwemo Naibu Katibu Mkuu Bara na Zanzibar, Katibu Mkuu Mnyika, Makamu Wenyeviti wa pande zote mbili, na Mwenyekiti Lissu) kwa lengo la kufikisha ujumbe wa “No Reforms No Election” kwa umma huku katika awamu ya pili, waandishi wa habari wakitolewa nje ili chama kibaki faragha na watia nia kujadiliana mambo ya ndani ya chama.

Mnyika ameeleza kuwa katika awamu ya kwanza, hotuba ya Lissu ilichukua takriban saa mbili kati ya saa tatu za awamu hiyo. Amesema katika hotuba hiyo, Lissu hakuzungumzia uasi bali alitoa darsa la kihistoria kuhusu madai ya mabadiliko ya kikatiba na kisheria tangu mwaka 1992, madhara ya mfumo mbovu wa uchaguzi wa mwaka 2020, na jinsi CHADEMA ilivyojaribu kufanya mazungumzo ya maridhiano na CCM baada ya uchaguzi huo.

Mnyika amethibitisha ushiriki wake katika mazungumzo ya maridhiano yaliyoanza Mei 22, 2022, baada ya Mwenyekiti wa wakati huo, Freeman Mbowe, kuachiwa kutoka gerezani na kukutana na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mnyika alikuwa miongoni mwa wajumbe 10 wa CHADEMA walioshiriki mazungumzo hayo. Walipendekeza “Minimal Reforms” (marekebisho madogo ya kikatiba na kisheria) kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 iwapo mchakato wa Katiba Mpya ungechelewa. Licha ya vikao kuendelea hadi Mei 31, 2023 chini ya timu za wataalamu zilizomhusisha Abdulrahman Kinana (CCM) na Freeman Mbowe (CHADEMA), upande wa CCM ulikataa mapendekezo yote kwa maandishi, jambo lililosababisha mazungumzo hayo kuvunjika kabisa.

Ushahidi wa Mnyika ulisimamishwa baada ya muda wa mahakama kuisha. Jopo la majaji limeahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu, Agosti 31, 2026, ambapo Katibu Mkuu huyo wa CHADEMA anatarajiwa kuendelea kutoa ushahidi wake wa utetezi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!