Mama na mtoto wake mwenye umri wa miaka mitatu wamefariki dunia baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto wakati wakiwa ndani, huku chanzo cha moto huo kikitajwa kuwa bado hakijafahamika.
Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 9 mchana katika Mtaa wa Kizota, Jijini Dodoma, ambapo mume wa marehemu na baba wa mtoto, Joshua Mawona, amesema alipigiwa simu na kupewa taarifa kuwa nyumba yake ilikuwa ikiteketea kwa moto. Alipofika eneo la tukio, alikuta moto mkubwa ukiwaka katika nyumba hiyo na kusababisha vifo vya familia yake.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema marehemu alikuwa amelala ndani ya nyumba hiyo kabla ya kusikia kelele na kutoka nje, lakini baada ya kuona moto ukiwaka katika dirisha, alirejea ndani kumfuata mtoto wake aliyekuwa bado amelala. Inadaiwa wakati akijaribu kutoka, mlango ulijifunga huku moto ukiwa umeenea, na hivyo kushindwa kutoka pamoja na mtoto wake hadi walipopoteza maisha.
Aidha Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma, Mrakibu (SF) Rehema Menda, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi wa kubaini chanzo cha moto bado unaendelea, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa haraka pindi wanapobaini kutokea kwa majanga ya moto ili hatua za uokoaji zichukuliwe kwa wakati.
