Latest Posts

SERIKALI YALENGA KUZIFIKIA KAYA MPYA 575,000 MPANGO WA TASAF

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege Qwaray, amesema utekelezaji wa programu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeleta mabadiliko katika maisha ya wananchi kwa kuwawezesha kaya zilizokuwa maskini kupata fursa za kuboresha maisha na kujitegemea.

Qwaray aliyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua mradi wa TASAF katika Shule ya Sekondari Fazilibucha, ambapo alisema programu hiyo imewasaidia wanufaika katika maeneo mbalimbali nchini kusomesha watoto, kujenga nyumba na kukidhi mahitaji muhimu ya familia, ikiwemo chakula na matibabu.

Alisema takribani wananchi milioni 1.3 wamewahi kunufaika na programu hiyo, huku zaidi ya kaya 400,000 zikifikia hatua ya kujitegemea baada ya kunufaika na miradi mbalimbali inayotekelezwa kupitia TASAF.

Qwaray alisema Serikali inalenga kuwafikia kaya 575,000 katika kipindi kijacho, hatua ambayo itasaidia kuongeza wigo wa wananchi watakaonufaika na programu hiyo.

Akikagua jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Fazilibucha, Qwaray alipongeza utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda na kutunza miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

Alisema uwepo wa majengo bora katika shule unasaidia kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu na watumishi wengine, jambo linalochangia katika utoaji wa huduma bora za elimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashimu Komba, alisema TASAF imewezesha utekelezaji wa miradi takribani 56 katika wilaya hiyo.

Alisema Manispaa ya Geita pekee imepata miradi 30, ambapo miradi 24 imeelekezwa katika sekta ya elimu na sita katika sekta ya afya, akieleza kuwa miradi hiyo imepokelewa vizuri na wananchi.

Jengo la utawala la Shule ya Sekondari Fazilibucha limegharimu Sh milioni 144 na limetekelezwa kupitia TASAF chini ya Mpango wa Kupunguza Umaskini Nchini Awamu ya Nne (TPRP IV).

Mkuu wa shule hiyo alisema jengo hilo limeboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa walimu na watumishi wa shule hiyo, huku Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwatulole, Edward Msalaba, akiahidi kuwa jamii itaendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda na kutunza miundombinu hiyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!