Latest Posts

BOOST YAFUTA KERO YA MADARASA BUZANAKI

Sekta ya elimu katika Kata ya Nyamalimbe, Wilaya ya Geita, Mkoa wa Geita imeendelea kuimarika kufuatia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kupitia programu ya BOOST, ikiwamo ujenzi wa madarasa matano katika Shule ya Msingi Buzanaki, Jimbo la Busanda.

Akizungumza mapema leo  kuhusu mradi huo, Mtendaji wa Kijiji cha Buzanaki amesema wananchi wameupokea kwa matumaini makubwa, wakieleza kuwa ujenzi wa madarasa hayo utasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa na msongamano wa wanafunzi shuleni.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Buzanaki, Lumaje Eliasi, amesema ujenzi wa madarasa hayo ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi pamoja na walimu.

Amesema kabla ya utekelezaji wa mradi huo, shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa, hali iliyokuwa ikiathiri mazingira ya ujifunzaji.

Diwani wa Kata ya Nyamalimbe, Lucas Madeni, amesema awali shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na upungufu mkubwa wa madarasa, lakini jitihada zinazofanyika katika kuboresha miundombinu ya elimu zimeanza kutoa matokeo chanya.

Madeni amesema juhudi za Mbunge wa Jimbo la Busanda katika kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya elimu zimechochea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu katika maeneo ya jimbo hilo.

Naye Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Busanda, Philip Mwanwari, amesema lengo la mbunge ni kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta ya elimu zinapatiwa ufumbuzi.

Mwanwari amesema elimu ni moja ya maeneo muhimu yanayohitaji kipaumbele, hivyo mbunge ataendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wananchi kuhakikisha kero za miundombinu ya shule zinaondolewa.

Amesema ujenzi wa madarasa hayo utakapokamilika utasaidia kuongeza nafasi za wanafunzi na kuweka mazingira bora zaidi ya kujifunza na kufundishia katika Shule ya Msingi Buzanaki.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!