Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amegoma kuweka jiwe la msingi katika Mradi wa Maji Kinyamburi, Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara, baada ya kutoridhishwa na ubora wa utekelezaji wa mradi huo.
Mhandisi Kundo amechukua hatua hiyo Oktoba 7, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Manyara, akisema Serikali haiwezi kuruhusu mradi unaotekelezwa kwa fedha za wananchi kukabidhiwa au kuzinduliwa wakati haujakidhi viwango vinavyotakiwa.
Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri amemuelekeza mkandarasi kurejea eneo la mradi na kufanya maboresho, ikiwemo kujenga upya sehemu ambazo hazijatekelezwa kwa kiwango kinachokubalika, ili kuhakikisha mradi huo unakuwa na ubora unaostahili.
Amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wa Kinyamburi wanapata huduma ya maji safi na salama kupitia miundombinu bora, imara na inayoweza kudumu kwa muda mrefu.
Mhandisi Kundo amesisitiza kuwa Wizara ya Maji itaendelea kusimamia kwa karibu miradi inayotekelezwa nchini na haitasita kuchukua hatua pale ambapo kazi hazifanywi kwa mujibu wa viwango na mikataba, akisisitiza kuwa fedha za Serikali lazima zitoe thamani halisi kwa wananchi.
