Kikundi cha vijana cha Tuinuane kilichopo Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, kimepatiwa trekta lenye thamani ya Shilingi milioni 100 linaloambatana na jembe na trela la tani tano, kupitia mpango mkakati wa programu ya Shilingi bilioni 200 chini ya Ofisi ya Rais- Maendeleo ya Vijana, hatua inayolenga kuongeza tija katika uzalishaji wa mahindi na kuboresha shughuli za kiuchumi za vijana hao.

Uwezeshaji huo wa kihistoria umekabidhiwa rasmi wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2026. Akizungumza katika ufunguzi wa wiki hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, ameeleza kuwa rasilimali hizo ni uthibitisho wa dhati wa utekelezaji wa ahadi za Serikali za kuwainua vijana kiuchumi kupitia sekta ya kilimo, huku akibainisha kuwa maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kuwawezesha vijana kugundua fursa zilizopo kwenye maeneo ya ufundi, biashara, elimu, na teknolojia.
Waziri Nanauka ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha na kuimarisha uratibu wa programu za vijana kwa kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo, ili kuhakikisha habari sahihi za mikopo, ajira, na mafunzo zinawafikia walengwa kwa wakati. Jitihada hizi zinasindikizwa na uzinduzi wa mfumo maalum wa kidijitali wa Youth Programme System unaorahisisha ufikiaji wa fursa hizo.
Maadhimisho ya Wiki ya Vijana mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu “Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana”, na yanahitimishwa kuelekea kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kinachotarajiwa kufanyika Oktoba 14, 2026.