Waziri wa Katiba na Sheria, Abdallah Hamis Ulega ametoa maagizo kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka akisisitiza umuhimu wa watendaji kufanya kazi kwa bidii, weledi, na ufanisi wa hali ya juu ili kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa haki nchini.
Akizungumza leo Oktoba 13, 2026 katika kikao chake cha kujitambulisha kwenye ofisi hizo zilizoko Njedengwa jijini Dodoma, Waziri Ulega ameelekeza kuwa ni lazima maagizo ya viongozi wakuu wa serikali na mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande yafanyiwe kazi kwa vitendo usiku na mchana.

Amesisitiza kuwa kesi lazima zifikishwe mahakamani kwa wakati na watuhumiwa wanaostahili wapatiwe dhamana kisheria ili kupunguza wimbi la msongamano mkubwa wa mahabusu gerezani.
Aidha, Waziri Ulega ameeleza kufurahishwa kwake na ongezeko la watendaji wa mashtaka kutoka 630 hadi kufikia 1,200, akabainisha kuwa ongezeko hilo linapaswa kuendana na kasi mpya ya utendaji kazi na kuleta matokeo chanya yanayoonekana. Sambamba na hayo, amevitaka vitengo vya elimu kwa umma kuongeza nguvu katika kutoa uelewa kwa wananchi kuhusu vigezo na taratibu za kisheria za dhamana, hatua itakayosaidia kupunguza malalamiko na kujenga imani kubwa ya umma kwenye vyombo vya utoaji haki.
“Ni lazima tufanye kazi usiku na mchana kwa kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande na maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Serikali, ili kuhakikisha kesi zinashughulikiwa na kufikishwa mahakamani kwa wakati, na watuhumiwa wanaostahili wanapata dhamana kwa mujibu wa sheria. Lengo letu ni kupunguza msongamano wa mahabusu na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati,” amesema Waziri Ulega.