Wajasiriamali walionufaika na mikopo ya asilimia 10 isiyokuwa na riba katika Manispaa ya Kibaha wametakiwa kurejesha fedha walizokopa kwa wakati ili kuwezesha vikundi vingine kupata mikopo hiyo na kujiendeleza kiuchumi.
Wito huo umetolewa leo na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Nicas Mawazo, alipokutana na vikundi vya wajasiriamali kutoka Kata ya Tangini vilivyonufaika na mikopo hiyo, akisema urejeshaji wa fedha kwa wakati ni muhimu ili fedha hizo ziendelee kutumika kuwasaidia wananchi wengine.

Amesema amefurahishwa na vikundi vilivyopata mikopo katika awamu iliyopita na kufanikiwa kurejesha fedha hizo kwa wakati, huku baadhi yake vikiomba tena mikopo katika dirisha jipya. Hata hivyo, amesisitiza kuwa vikundi vinavyopata mikopo vinapaswa kutimiza wajibu wa kurejesha fedha hizo ili visiwe kikwazo kwa wengine wanaohitaji fursa hiyo.
Aidha, amevitaka vikundi hivyo kujisajili BRELA na kuwa kampuni pamoja na kujiunga na mfumo wa NEST ili viweze kushiriki katika zabuni zinazotangazwa na Halmashauri, akieleza kuwa sheria inaelekeza asilimia 30 ya zabuni kutolewa kwa wazawa.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo wa Manispaa ya Kibaha, Mkaminoela Hangaya, amesema vikundi 120 vimepitishwa katika dirisha hili kwa ajili ya kupatiwa mikopo hiyo, huku mchakato ukizingatia wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
