Latest Posts

BUNGE LAPONGEZA UJENZI WA BIRIKA LA MIFUGO SANGASANGA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imepongeza juhudi za Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu katika ujenzi wa mradi wa birika la kunyweshea mifugo katika Kijiji cha Sangasanga, Vitongoji vya Masanze na Lubungo, Wilaya ya Morogoro.

Mradi huo unalenga kulinda vyanzo vya maji dhidi ya uchafuzi na uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu, hususan mifugo kuingia moja kwa moja kwenye vyanzo.

Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Patrick Mwalunenge, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi. Mhe. Mwalunenge amewataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Amesema upatikanaji wa maji kwa mifugo katika maeneo maalumu ni hatua muhimu ya kupunguza athari za ufugaji unaofanyika ndani na pembezoni mwa vyanzo vya maji, na hivyo miundombinu iliyojengwa itunzwe kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Akitoa maelezo ya mradi, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmassy, amesema mradi huo umejengwa kwa lengo la kupunguza athari za mifugo katika vyanzo vya Mto Mlali na Bwawa la Mindu.

Mhandisi Mmassy amebainisha kuwa mradi unatekelezwa na wataalamu wa ndani kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wa World Waternet, na umegharimu shilingi milioni 65.

Ameeleza kuwa mradi unahusisha uchimbaji wa kisima chenye urefu wa mita 110, ufungaji wa mfumo wa nishati ya jua, ujenzi wa mnara wa tenki la maji pamoja na mtandao wa mabomba wenye urefu wa mita 54.

Aidha, mradi umejumuisha ujenzi wa kituo cha kuchotea maji chenye koki mbili kwa ajili ya wananchi, pamoja na birika lenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 5.8 za maji, ambalo linaweza kunywesha mifugo takribani 50 kwa wakati mmoja ndani ya dakika 15.

Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Sangasanga wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka kipaumbele katika miradi ya maji inayolenga kuboresha maisha ya wananchi, kuimarisha ufugaji na kulinda mazingira.

Wamesema mradi huo utawasaidia kupata huduma ya maji kwa urahisi, kupunguza changamoto ya mifugo kutafuta maji kwenye vyanzo vya asili na kuimarisha ushirikiano kati ya wakulima na wafugaji.

Mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba hadi Desemba 2026, ukiwa sehemu ya juhudi za Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu katika kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za maji kwa maendeleo endelevu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!