Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kurahisisha taratibu za upatikanaji wa mikopo kwa wanawake kwa kuwaondolea vikwazo visivyo vya lazima vinavyochelewesha huduma hiyo.
‎Mahundi ametoa agizo hilo Novemba 12, 2026, wakati akifungua Kongamano la Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi mkoani Mbeya, akisisitiza kuwa maafisa hao wanapaswa kuwa karibu na wanawake, kuwapatia maelekezo sahihi na kuwasaidia kukamilisha hatua za maombi ya mikopo kwa wakati.
‎
‎Amesema uwezeshaji wanawake kiuchumi unahitaji kuwapatia fursa, rasilimali, ujuzi, mitaji na teknolojia zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za biashara, kilimo, viwanda na sekta nyingine zinazozalisha kipato.
‎Ameongeza kuwa makongamano yanayoandaliwa yanapaswa kuwa majukwaa ya kukumbushana wajibu wa kuwahudumia wananchi badala ya kufanyika kama utaratibu wa kawaida usioleta matokeo.
‎
‎Aidha, Mahundi amesema pamoja na hatua zilizopigwa, wanawake bado wanakabiliwa na changamoto za kupata mikopo, mitaji na mazingira rafiki ya kufanya biashara, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuimarisha mifumo ya kifedha.
‎Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Jumanne Sagini, amesema utoaji wa elimu kuhusu uwezeshaji wanawake kiuchumi ni muhimu katika kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kushiriki katika maendeleo.
‎
‎Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi mkoani humo, Neema Kisanga, amewasilisha maoni ya jukwaa kuhusu kuendeleza juhudi za kuwawezesha wanawake, huku kongamano hilo likiwakutanisha viongozi, wadau na wajasiriamali kujadili fursa na changamoto za kiuchumi.