Latest Posts

CWT YAWAFARIJI WALIMU WALIOPOTEZA MAKAZI KWA MOTO CHATO

Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Geita kimewafariji walimu wawili waliokumbwa na majanga ya moto yaliyoteketeza nyumba zao katika Kata ya Buseresere, Wilaya ya Chato mkoani Geita, kwa kuwapatia msaada wa vifaa vya ujenzi vyenye lengo la kuwasaidia kurejesha makazi yao.

Katika msaada huo, Mwalimu Nkwabi Mathias amekabidhiwa mifuko 30 ya saruji, huku Mwalimu Hassan Saidi akipatiwa mabati 36 kwa ajili ya kusaidia ujenzi na ukarabati wa nyumba zao.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo mapema leo , Katibu wa CWT Mkoa wa Geita, Pauline Tinda, alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa chama katika kuhakikisha wanachama wake wanapata faraja na msaada wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali.

Alisema juhudi zinazofanywa na viongozi wa CWT Wilaya ya Chato katika kubaini matatizo yanayowakabili walimu na kuweka utaratibu wa kuyashughulikia zinastahili kupongezwa, huku akiwataka kuendelea na juhudi hizo bila kuchoka.

Alieleza kuwa CWT itaendelea kusimamia masilahi ya walimu kwa kutoa huduma za utetezi, msaada wa kijamii na kisheria, pamoja na kufuatilia changamoto zao kwa waajiri.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Chato, Mwalimu Kibinti Frank, alisema mbali na jukumu la kutetea haki na masilahi ya walimu, chama hicho kimekuwa kikitoa huduma za kijamii kwa kuwafikia wanachama wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali.

Kwa upande wao, walimu waliopatiwa msaada huo walikishukuru chama kwa kuwafikia na kuwapatia vifaa hivyo, wakisema hatua hiyo imewapa faraja na kuonesha mshikamano wa chama katika kipindi kigumu wanachopitia.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!