Serikali imeendelea kuimarisha huduma za afya kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, kwa kuongeza idadi ya wodi maalumu za uangalizi na matibabu ya watoto wachanga (NICU) kutoka 14 mwaka 2018 hadi kufikia 438 mwaka 2026, hatua inayolenga kuokoa maisha ya watoto hao na kuwapa nafasi ya kukua na kustawi.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti Duniani yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mkoani Geita mapema leo , Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema ongezeko hilo limechangia pia kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaopata huduma katika wodi hizo kutoka 30,562 hadi 64,007.
Amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya huduma hizo kwa kushirikiana na wadau, ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kujenga wodi 100 za kisasa za NICU ifikapo Julai 2028, ambapo wodi 36 tayari zipo katika hatua za ujenzi, huku nyingine zikiendelea na hatua mbalimbali za maandalizi katika ngazi za mikoa na halmashauri.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Watoto Tanzania, Dkt. Theopista Jacob Masenge, amesema takwimu zinaonesha kuwa katika kila watoto 10 wanaozaliwa, mtoto mmoja huzaliwa kabla ya kutimiza wiki 37 za ujauzito, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuwekeza katika huduma za afya kwa watoto hao.
Aidha, baadhi ya wazazi waliojaliwa kupata watoto njiti wametoa ushuhuda wa changamoto walizokutana nazo pamoja na namna huduma za afya zilivyowasaidia watoto wao kupata matibabu na uangalizi maalumu.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mjini Geita, yamebeba kaulimbiu isemayo: “Watoto waliozaliwa kabla ya wakati wana uwezo mkubwa wa kukua na kustawi. Tuwekeze katika huduma na ufuatiliaji wao ili kuilinda kesho yao.”