Mradi wa Forestry, Land Use, and Value Chains Development in Tanzania (FORLAND Tanzania) umeendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya misitu nchini kwa kuwakutanisha katika majadiliano yanayolenga kuboresha ubora na kuongeza thamani ya mazao ya misitu, hususan mbao, katika mnyororo mzima wa thamani kuanzia uzalishaji hadi kumfikia mlaji wa mwisho.
Majadiliano hayo yaliyofanyika katika Hoteli ya Sunset yamelenga kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa wadau kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora katika uzalishaji na biashara ya mazao ya misitu, ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakuwa na ubora unaokidhi mahitaji ya soko na kuongeza ushindani wake.
Akizungumza katika majadiliano hayo, Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa FORLAND kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Emma Nzunda, amesema mradi huo umekuwa ukishirikiana kwa karibu na Wizara, taasisi zake pamoja na halmashauri katika kuhamasisha uzingatiaji wa viwango vya ubora wa mbao kuanzia hatua ya upandaji miti hadi uvunaji.
Amesema ni muhimu kuzingatia ubora katika kila hatua ya mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu, kwani hatua hizo zina mchango mkubwa katika kuhakikisha mbao zinazozalishwa zinakuwa na ubora unaotakiwa na hivyo kuongeza thamani yake katika soko.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa FORLAND Mkoa wa Iringa, Nyachia Robert, amesema majadiliano hayo yanalenga kuongeza uelewa kwa jamii na wadau kuhusu umuhimu wa ubora na thamani ya mbao katika mnyororo mzima wa biashara, kuanzia kwa mkulima anayezalisha miti hadi kwa mlaji wa mwisho.
Ameeleza kuwa kupitia majadiliano hayo, wadau wanapata fursa ya kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mbalimbali na kuelewa namna bora ya kuboresha shughuli zao katika uzalishaji na biashara ya mazao ya misitu, ili kuongeza thamani ya bidhaa zao na kunufaika zaidi na fursa zilizopo katika sekta hiyo.

Wakitoa maoni yao, wadau walioshiriki majadiliano hayo wameushukuru mradi wa FORLAND kwa kuwawezesha kupata maarifa na mbinu mbalimbali zitakazowasaidia kuboresha shughuli zao za kibiashara, hususan katika kuhakikisha mazao ya misitu yanazalishwa kwa kuzingatia ubora na kufikishwa sokoni yakiwa na thamani inayostahili.
Wamesema elimu na uzoefu walioupata kupitia majadiliano hayo ni muhimu katika kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu, kuanzia uzalishaji hadi soko la mwisho, huku wakieleza kuwa ushirikiano wa wadau ni nyenzo muhimu katika kukuza sekta ya misitu na kuongeza manufaa ya kiuchumi yatokanayo na rasilimali hiyo nchini.
