Latest Posts

RELI YA TAZARA KUWA MHIMILI MPYA WA UCHUMI WA UKANDA WA SADC

 

Na Mwandishi Wetu

Uwekezaji wa kihistoria uliofanywa na China katika reli ya TAZARA umetajwa kuifufua reli hiyo kwa usafirishaji wa tani milioni 2.4 za mizigo kwa mwaka, kuimarisha biashara ya Tanzania, Zambia na DRC, huku Bandari ya Dar es Salaam ikitarajiwa kunufaika zaidi.

 

Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), iliyojengwa kama alama ya urafiki na mshikamano kati ya Tanzania, Zambia na China, inaelekea kuandika ukurasa mpya wa historia yake kupitia mradi mkubwa wa ufufuaji na uboreshaji unaolenga kuibadilisha kutoka miundombinu inayokabiliwa na changamoto za kiutendaji na kiusalama na kuwa mhimili muhimu wa usafirishaji, biashara na maendeleo ya uchumi wa kikanda.

 

Baada ya miaka 50 tangu reli hiyo ilipoanza rasmi kutoa huduma mwaka 1976, hatua ya sasa ya kuifufua inaashiria dhamira ya kurejesha hadhi yake ya kihistoria, kuimarisha uwezo wake wa kiutendaji na kuifanya kuwa njia muhimu zaidi ya kusafirisha abiria na mizigo kati ya nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na masoko ya kimataifa.

 

Huu si mradi wa kawaida wa kufanya matengenezo ya miundombinu ya reli, bali ni mpango mpana wa kurejesha uwezo wa reli hiyo kufanya kazi kwa ufanisi, usalama na kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ya biashara na usafirishaji.

 

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ufufuati ya TAZARA, Zhang Zhenhai, alisema wa Ufufuaji wa Reli ya TAZARA ni mpango mkubwa zaidi wa ukarabati na uboreshaji wa reli hiyo tangu ilipokabidhiwa na kuanza kutoa huduma mwaka 1976.

 

Alisema mradi huo unahusisha mtandao wa reli wenye urefu wa kilomita 1,860.543 unaopita katika nchi za Tanzania na Zambia, huku utekelezaji wake ukifanyika kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).

 

Mfumo huo unalenga kuunganisha uwezo, uzoefu na rasilimali za pande zinazohusika ili kuhakikisha reli inafufuliwa na kuendeshwa kwa misingi ya usalama, ufanisi na uendelevu wa kibiashara.

 

Moja ya malengo makubwa ya mradi huo ni kukabiliana na changamoto za muda mrefu ambazo zimekuwa zikiathiri ufanisi wa reli hiyo, ikiwemo uchakavu wa miundombinu, maeneo yanayolazimu treni kupunguza mwendo na vihatarishi mbalimbali vya kiusalama.

 

Changamoto hizo zimekuwa na athari katika uwezo wa reli kusafirisha mizigo kwa wakati, kuongeza safari na kukidhi mahitaji ya wateja wanaotegemea huduma zake.

 

Katika kutekeleza mradi huo, kipaumbele cha awali ni kufanya matengenezo muhimu na kuondoa vihatarishi vikubwa vya usalama ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya ujenzi.

 

Zhang alifafanua kuwa baada ya kukamilika kwa hatua hiyo, kazi nyingine za ukarabati na uboreshaji zitaendelea katika kipindi cha uendeshaji, kwa awamu kulingana na mahitaji na mazingira yatakavyoruhusu.

 

Mkakati huo unaonyesha kuwa ufufuaji wa TAZARA hautaishia katika ukarabati wa awali, bali utakuwa mchakato endelevu wa kuimarisha miundombinu na uwezo wa reli hiyo kadiri mahitaji ya usafirishaji yatakavyoongezeka.

 

Katika hatua hiyo, maeneo yanayohusisha hali ya ardhi, njia za reli, madaraja na vichuguu yatafanyiwa kazi ili kuondoa vihatarishi vinavyoweza kuhatarisha usalama wa safari za treni.

 

Lengo ni kurejesha reli katika viwango vya uendeshaji vilivyokusudiwa tangu ilipojengwa, hatua itakayowezesha kuongeza ufanisi wa safari na kupunguza vikwazo vinavyosababisha ucheleweshaji wa usafirishaji.

Kwa maana hiyo, mafanikio ya mradi hayatapimwa kwa kiasi cha miundombinu itakayokarabatiwa pekee, bali pia uwezo wa reli kutoa huduma za uhakika, salama na zenye ushindani katika soko la usafirishaji.

 

MIZIGO KUONGEZEKA HADI TANI MILIONI 2.4

Moja ya matarajio makubwa ya ufufuaji wa TAZARA ni kuongeza kwa kiwango kikubwa uwezo wa kusafirisha mizigo, jambo litakaloiwezesha reli hiyo kuchukua nafasi muhimu zaidi katika mnyororo wa biashara na usafirishaji wa kikanda.

 

Kwa mujibu wa Zhang, baada ya kukamilika kwa mradi, reli hiyo inatarajiwa kuendesha huduma za usafirishaji wa makontena kwa ratiba maalumu kati ya New Kapiri Mposhi nchini Zambia na Kurasini jijini Dar es Salaam.

 

Huduma hiyo itahusisha usafirishaji wa madini ya shaba na bidhaa nyingine, kwa kuzingatia mahitaji ya soko na biashara.

 

Muhimu zaidi, uwezo wa kusafirisha mizigo kwa mwaka unatarajiwa kuongezeka kutoka takribani tani 200,000 za sasa hadi tani milioni 2.4.

Hiyo ni ongezeko kubwa linaloonyesha matarajio ya kuibadilisha TAZARA kuwa njia muhimu ya usafirishaji wa mizigo ya kibiashara, hasa kwa nchi zisizo na bandari zinazotegemea miundombinu ya nchi jirani kufikisha bidhaa zao katika masoko ya kimataifa.

 

Ongezeko hilo likifikiwa, litafungua fursa mpya kwa wafanyabiashara, wazalishaji, kampuni za uchimbaji madini na wadau wengine wa sekta ya usafirishaji.

 

Aidha, huduma za makontena kwa ratiba maalumu zitakuwa na umuhimu katika kuongeza uhakika wa usafirishaji, kupunguza changamoto za kupanga safari za mizigo na kuwapa wafanyabiashara mazingira bora ya kupanga shughuli zao.

 

Kwa Tanzania, ongezeko la mizigo kupitia TAZARA linaweza kuongeza shughuli za kiuchumi zinazohusiana na usafirishaji, uhifadhi wa bidhaa, huduma za bandari na biashara zinazozunguka miundombinu hiyo.

 

BANDARI YA DAR ES SALAAM KUWA KITOVU MUHIMU ZAIDI

Katika mustakabali wa mradi huo, Bandari ya Dar es Salaam inatajwa kuwa miongoni mwa miundombinu itakayoweza kunufaika na ufufuaji wa TAZARA.

 

Hii inatokana na nafasi ya reli hiyo katika kuunganisha maeneo ya uzalishaji wa bidhaa na madini nchini Zambia na maeneo ya kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na bandari hiyo.

 

Kwa sasa, ushindani wa bandari katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini unazidi kuongezeka, huku nchi mbalimbali zikiimarisha miundombinu ya usafirishaji ili kuvutia mizigo ya kimataifa.

Katika mazingira hayo, kuwa na reli yenye uwezo wa kusafirisha mizigo kwa ufanisi ni moja ya nyenzo muhimu zinazoweza kuongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam.

 

TAZARA inapofanya kazi kwa ufanisi, inakuwa sehemu muhimu ya mfumo wa usafirishaji unaounganisha reli na usafiri wa baharini.

 

Muunganiko huo utatoa fursa ya kusafirisha bidhaa kutoka maeneo ya ndani ya nchi hadi bandarini, ambako zitaendelea na safari zake kwenda katika masoko mbalimbali ya kimataifa.

 

Kwa upande mwingine, bidhaa zinazoingia kupitia Bandari ya Dar es Salaam zinaweza kusafirishwa kwa reli kwenda katika masoko ya ndani ya Tanzania na nchi jirani.

Hivyo, TAZARA inatarajiwa kuwa kiungo muhimu katika kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la biashara na usafirishaji kwa nchi za ukanda huo.

 

FURSA MPYA KWA ZAMBIA NA DRC

Umuhimu wa TAZARA hauishii katika mipaka ya Tanzania na Zambia pekee, bali unagusa pia uchumi wa nchi nyingine zinazotegemea njia za usafirishaji kupitia ukanda huo.

 

Zhang anasema reli hiyo iliyofufuliwa itakuwa na mchango mkubwa katika kusafirisha madini yanayozalishwa nchini Zambia na maeneo ya kusini mwa DRC kwenda katika masoko ya kimataifa kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

 

Hili linaifanya TAZARA kuwa na nafasi ya kimkakati katika biashara ya madini, hususan shaba, ambayo ni miongoni mwa rasilimali muhimu katika uchumi wa nchi hizo.

 

Kwa kuwa madini ni bidhaa zinazohitaji mifumo madhubuti ya usafirishaji kutoka maeneo ya uzalishaji hadi kwenye masoko ya kimataifa, uwepo wa reli yenye uwezo mkubwa wa kubeba mizigo unaweza kuongeza ufanisi wa mnyororo mzima wa biashara hiyo.

 

Aidha, usafirishaji wa uhakika unaweza kusaidia kupunguza vikwazo vya kiutendaji vinavyoweza kujitokeza katika mchakato wa kupeleka bidhaa bandarini.

 

Kwa mtazamo mpana, ufufuaji wa TAZARA unaweza kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania, Zambia na DRC, huku ukifungua fursa za uwekezaji katika maeneo yanayopitiwa na reli hiyo.

 

HUDUMA ZA ABIRIA KUENDELEA KUWA MUHIMU

Pamoja na msisitizo mkubwa unaowekwa katika usafirishaji wa mizigo, TAZARA haitapoteza jukumu lake la kihistoria la kutoa huduma za usafiri kwa wananchi.

 

Kwa mujibu wa Zhang, reli hiyo itaendelea kutoa huduma za abiria kwa ratiba maalumu, sambamba na huduma za usafirishaji wa bidhaa muhimu kwa jamii zinazoishi katika maeneo inayopitia.

 

Hili ni jambo muhimu kwa wananchi wanaotegemea reli hiyo katika shughuli zao za kila siku, ikiwemo safari za kibiashara, kijamii na shughuli nyingine za kiuchumi.

 

Huduma za abiria zenye ratiba zinazotabirika zinaweza kuongeza uhakika wa safari na kuimarisha muunganiko kati ya jamii mbalimbali zinazopitiwa na reli hiyo.

 

Aidha, kuimarika kwa huduma za reli kunaweza kuchochea shughuli za kiuchumi katika miji na vituo vilivyopo kando ya njia hiyo, kupitia biashara ndogondogo, huduma za malazi na shughuli nyingine zinazohusiana na usafiri.

 

Kwa mantiki hiyo, mafanikio ya ufufuaji wa TAZARA yanapaswa kuonekana katika pande mbili; kuongeza uwezo wa kibiashara wa reli na wakati huohuo kuendelea kuhudumia wananchi.

 

MFUMO WA UBIA NA UENDELEVU WA UENDESHAJI

Katika kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa, ushirikiano kati ya TAZARA na kampuni itakayohusika na uendeshaji kupitia mkataba wa ubia una umuhimu mkubwa.

 

Zhang alisema TAZARA na kampuni hiyo zitafanya kazi kwa karibu kwa kutumia uwezo na uzoefu wa kila upande, huku zikiweka utaratibu utakaowezesha reli kuendeshwa kwa usalama na uendelevu wa muda mrefu.

 

Hili ni eneo muhimu kwa sababu mafanikio ya mradi mkubwa wa miundombinu hayaishii katika kukamilisha kazi za ujenzi na ukarabati, bali pia yanategemea uwezo wa kusimamia, kutunza na kuendesha miundombinu hiyo baada ya kukamilika.

 

Kwa hiyo, ushirikiano huo unatarajiwa kuweka msingi wa uendeshaji unaozingatia mahitaji ya wateja, usalama wa safari, ubora wa huduma na uwezo wa kibiashara wa reli.

 

Hata hivyo, utekelezaji wake utahitaji uwajibikaji wa pande zote, usimamizi madhubuti wa mkataba na kuhakikisha kuwa maslahi ya kiuchumi yanaenda sambamba na wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi.

 

TAZARA RAILWAY PROSPERITY BELT: DIRA YA MAENDELEO YA UKANDA

Mbali na kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji wa mizigo, mradi huo una matarajio mapana zaidi ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo yanayopitiwa na reli.

 

Zhang alibainisha kuwa TAZARA iliyofufuliwa itachangia maendeleo ya ukanda wa kiuchumi unaojulikana kama TAZARA Railway Prosperity Belt.

 

Dhana hiyo inaonyesha matarajio ya kutumia uwepo wa reli kama kichocheo cha shughuli mbalimbali za kiuchumi na uwekezaji katika maeneo yanayozunguka miundombinu hiyo.

 

Kwa kawaida, miundombinu ya usafiri inapoboreshwa, huongeza fursa za kuanzishwa na kukua kwa shughuli za biashara, viwanda, maghala, vituo vya usambazaji wa bidhaa na huduma nyingine zinazohitaji usafiri wa uhakika.

 

Katika muktadha huo, TAZARA inaweza kuwa kichocheo cha kuimarisha shughuli za uzalishaji na biashara katika maeneo inayopitia, badala ya kubaki njia ya kupitisha treni pekee.

 

Hata hivyo, kufikiwa kwa matarajio hayo kutahitaji mipango madhubuti ya uwekezaji, ushirikishwaji wa sekta binafsi na uratibu wa sera za maendeleo kati ya Tanzania na Zambia.

 

URAFIKI WA TANZANIA, ZAMBIA NA CHINA KUPEWA MAANA MPYA

TAZARA ni zaidi ya reli ya kusafirisha abiria na mizigo. Ni alama ya ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania, Zambia na China, iliyojengwa katika kipindi ambacho nchi hizo zilikuwa na dhamira ya kuimarisha uhusiano na maendeleo ya kiuchumi.

 

Kupitia mradi wa sasa wa ufufuaji, historia hiyo inaelekea kupewa maana mpya, kwa kuifanya reli hiyo kuwa miundombinu inayoweza kuhimili mahitaji ya uchumi wa kisasa.

 

Zhang alisema reli iliyofufuliwa itaendelea kuwa alama ya urafiki wa China na Afrika, huku ikibadilika na kuwa reli kuu yenye uwezo wa kujiendesha kibiashara na kuhudumia usafirishaji wa abiria na mizigo.

 

Kauli hiyo inaonyesha kuwa lengo si kuhifadhi historia ya TAZARA pekee, bali pia kuhakikisha inakuwa na nafasi muhimu katika mustakabali wa uchumi wa nchi zinazohusika.

 

Tanzania na Zambia, hatua hiyo ni fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kutumia miundombinu ya pamoja kama nyenzo ya kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo ya wananchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!