Mtia nia ya ubunge jimbo jipya la Uyole jijini Mbeya Wailes Malongo, ametangaza nia yake ya kugombea ubunge jimbo jipya la Uyole kupitia ACT Wazalendo akisema ni jimbo lililotengwa kimaendeleo hasa kwenye miundombinu ya barabara na ukosefu wa kutosha wa huduma ya maji safi.
Mtia nia huyo wa ubunge jimbo la Uyole kupitia chama cha ACT Wazalendo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho jimbo la Mbeya mjini Wailes Malongo Mwachiso amesema hayo kwenye mahojiano yake na Jambo Tv jijini humo kuhusu dhamira yake ya kujitosa kwenda kupambana na wanasiasa wengine katika jimbo hilo akiwemo Dkt. Tulia Ackson ambaye ametangaza kuwania ubunge jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wailes Malongo Mwachiso amesema amejipima na kuona anatosha kuwa mbunge wa Jimbo la Uyole akisema hata ikiwa jimbo moja na Mbeya mjini lakini Uyole ilikuwa imetengwa kwani imesahaulika kimaendeleo hasa ukosefu wa kituo cha mabasi Uyole njiapanda, ubovu wa miundombinu ya barabara, ukosefu wa uhakika wa huduma ya maji safi na mengine kadha wa kadha aliyosema yatakuwa kipaumbele chake endapo atapitishwa na chama chake na kuchaguliwa na wananchi kuwa mbunge wa Jimbo la Uyole.
Alipoulizwa mchango wa Dkt. Tulia Ackson (Mbunge wa sasa wa Mbeya mjini kabla ya jimbo kugawanywa, mwanasiasa huyo kijana amejibu kuwa…
“Mchango wake ni asilimia kumi katika mia moja yaani asilimia tatu Uyole na asilimia saba Mbeya mjini kwahiyo hamna kitu alichofanya ni asilimia tatu Uyole ndio maana nasema Uyole wananchi walikuwa wametengwa, mimi nikiwa Mbunge tutashirikiana na wenzangu kutafuta eneo lingine kuwapeleka kilimo ili pale kilimo tufanye vitu vingine kilimo hapa mjini sio sawa, ukienda kule Isyesye, Itezi na maeneo mengine ambayo viwanja ni vya kupimwa barabara ni mbovu, maji ni shida hadi umeme ni kero”, ameeleza Wailes Malongo, mtia nia ya ubunge jimbo la Uyole ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo jimbo la Mbeya mjini.
Pamoja na hayo amewaomba wananchi kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa kuchagua viongozi kupitia Chama cha ACT Wazalendo akidai wamejipanga kushiriki uchaguzi mkuu kuhakikisha wanashinda hata kama sheria za uchaguzi sio rafiki hivyo wameshaanza kuandaa mawakala waaminifu ili kuhakikisha wanapambana na vyama vingine ikiwemo wapinzani wao wakubwa CCM.