Latest Posts

AFRIKA YAPANIA KUONGEZA UPATIKANAJI WA UMEME KWA WATU MILIONI 300

Tanzania imeandaa mkutano mkubwa wa viongozi wa nchi za Afrika kuhusu nishati, maarufu kama “Mission 300,” ambao umefunguliwa rasmi leo Januari 27, 2025.

Lengo kuu la mkutano huu ni kuharakisha upatikanaji wa umeme kwa Waafrika milioni 300 katika kipindi cha miaka mitano, hatua inayolenga kufungua fursa za maendeleo barani Afrika.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dkt. Doto Biteko, katika hotuba yake ya ufunguzi, amesisitiza umuhimu wa azma hii katika kutimiza Ajenda ya Afrika 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Ameeleza kuwa Tanzania, ambayo wakati wa uhuru mwaka 1960 ilikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 21 pekee, sasa inazalisha megawati 3,160, huku ikitarajia kufikia megawati 4,000 mwishoni mwa mwaka 2025. Hata hivyo, bado Waafrika milioni 571 hawana huduma ya umeme, jambo linalodhihirisha umuhimu wa mkutano huu.

Mkutano huu umbao unahudhuriwa na zaidi ya marais 25, mawaziri wa nishati, viongozi wa taasisi za kimataifa, na wadau wa sekta binafsi. Miongoni mwao ni Rais wa Benki ya Dunia (WB), Bw. Ajay Banga, aliyesema kuwa juhudi za pamoja zinaweza kuleta mapinduzi katika sekta ya nishati barani Afrika, kuhakikisha kuwa wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), Dkt. Akinumwi Adesina, ameisifu Tanzania kwa kuwa mfano wa mafanikio katika uwekezaji wa nishati vijijini, akisisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika kufanikisha malengo ya “Mission 300.”

Naye Waziri wa Fedha wa Zambia, Dkt. Situmbeko Musokotwane, ametoa shukrani kwa Tanzania kwa msaada wa nishati inayoiuzia Zambia, akibainisha kuwa ushirikiano wa kikanda katika sekta ya nishati ni muhimu kwa maendeleo ya Afrika nzima.

Mkutano huu pia unatarajiwa kujadili mbinu za kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi, kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, na kuzindua mfumo wa ufuatiliaji wa maazimio yatakayokubaliwa. Dkt. Biteko amebainisha kuwa Tanzania imeweka kipaumbele katika kuimarisha miundombinu ya umeme na kuunganisha nchi jirani kama Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, na Zambia.

Katika hotuba yake, Naibu Waziri Mkuu amewaomba washiriki wa mkutano kushirikiana katika kufanikisha maazimio ya mkutano huu, akisema kuwa upatikanaji wa nishati safi ni msingi wa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu barani Afrika.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!