Latest Posts

ASKOFU CHILONGANI AAGIZWA KUSIMAMIA MAADILI NA UBORA WA ELIMU

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Maimbo Mndolwa, amemtaka Mkuu mpya wa Chuo Kikuu cha St John, Askofu Dk. Dickson Chilongani, kusimamia kwa dhati maadili ya wanafunzi na ubora wa elimu ya juu, akitaka pia kuwepo kwa mjadala mpana juu ya sera ya kitaifa ya maadili.

Akizungumza katika ibada maalum ya kumsimika Dk. Chilongani kuwa Mkuu wa pili wa Chuo hicho, Askofu Mndolwa amesema hali ya mmonyoko wa maadili katika jamii inahitaji uongozi wa kielimu unaojikita katika misingi ya maadili, nidhamu na ubora wa maarifa.

“Sasa hivi tunajiuliza: sera ya maadili iko wapi? Viongozi wa vyuo vya Kikristo mnapaswa kuwa mstari wa mbele. Idara ya Theolojia haina budi kusonga mbele zaidi, si kufundisha tu, bali kuanza kupaza sauti kwenye hoja za kijamii,” alisema Askofu Mndolwa.

Askofu Dk. Chilongani, ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika, anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Askofu Mstaafu Leonard Mtetemela aliyeiongoza St. John tangu Septemba 8, 2007 – jumla ya miaka 18 ya utumishi.

 

Dk. Chilongani: Tutasimamia Maadili, Tutaongeza Ubora wa Mazingira ya Kujifunzia

Akizungumza mara baada ya kusimikwa, Askofu Dk. Chilongani amesema anapokea chuo hicho katika hali nzuri kitaaluma na ameahidi kushirikiana na viongozi na watumishi wa chuo hicho kupambana na changamoto mbalimbali, hasa za maadili na miundombinu.

“Tutahakikisha tunazalisha wahitimu wenye maadili, wenye maarifa na wanaotambulika katika jamii. Pia nitashughulikia kwa kina suala la ukosefu wa hosteli, ili wanafunzi wakae katika mazingira bora ya kujifunzia,” alisema.

Ibada hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kanisa, wasomi, wanafunzi na wadau wa elimu, ikiwa ni ishara ya kulipa uzito wa kipekee jukumu la uongozi wa taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na taasisi za kidini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!