Mhashamu Titus Mdoe Askofu wa Jimbo Katoliki Mtwara,amewaasa wazazi/walezi kulea na kuwakuza watoto na vijana kwenye maadili ya kumpendeza Mungu.
Hayo ameyaeleza Mei 31,2025 kwenye hitimisho la maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Parokia ya Mtakatifu Paul Majengo Jimbo Katoliki Mtwara tangu kuanzishwa kwake,Askofu Mdoe amesema tuna ya watoto na vijana wetu ni muhimu sana katika ustawi wa maisha yao hivyo amewaomba wazazi kuwatengenezee mazingira mazuri ili kuwa na vizazi vyenye misingi imara.
Amewataka pia waumini kuendelea kufuata njia za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi wa maisha yao ya kimwili ikiwemo upendo na mshikamano ndani ya familia zao, jumuhiya na taifa kwa jumla pamoja na kudumisha ushirikiano hadi nje ya kanisa kwa watu wote bila ubaguzi.
Ameongeza kuwa katika kusherehekea huko wanapata fursa wanakanisa hao na kama sehemu ya taifa kwa kuendelea kusali na kumwomba Mungu ili awaweke salama, kuwaleta karibu watanzania, awaondolee matatizo yasiyokuwa ya lazima katika nchi yao.
Kwa upande wao baadhi ya waumini wa Kanisa hilo ikiwemo Mwenyekiti wa Kigango cha Roho Mtakatifu Mangamba CPA Norbert Shee amesema katika mambo wanayopaswa kujifunza ikiwemo waumini kuanza kuelewa kwamba kujenga Kanisa ni jukumu lao na siyo kutegemea misaada kutoka kwa wengine huku akiwaomba kuendelea kueneza injili kwa imani na matendo yaliyokuwa mema.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Parokia ya Mtakatifu Paul Majengo, Jimbo Katoliki Mtwara ambapo Jubilei hiyo ilizinduliwa Aprili 14,2024.