Latest Posts

BOB CHACHA WANGWE NA MATUMAINI YA TUNDU LISSU KUFANYA MAGEUZI CHADEMA

Na; mwandishi wetu

Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bob Chacha Wangwe amesema ameamua kuweka wazi msimamo wake wa kwamba anamuunga mkono Tundu Lissu badala ya Freeman Mbowe katika mchakato wa kinyang’anyiro cha kumtafuta Mwenyekiti wa chama hicho Taifa kutokana na mahitaji ya sasa ya kisiasa yaliyopo hapa nchini ambayo anaamini mtu sahihi wa kuikomboa CHADEMA ni Lissu

Akihojiwa na Jambo TV, Ijumaa Januari 03.2024 Bob amesema katika nyakati hizi ambazo mazingira ya siasa na demokrasia ya Tanzania imeminywa kwa kiasi kikubwa hadi kufikia hatua ya kile alichodai uporaji wa chaguzi mbalimbali za Kitaifa, uwepo wa matukio ya utekaji na mauaji hasa kwa wafuasi wa chama hicho, uwepo wa tuhuma za rushwa miongoni mwa viongozi waandamizi wa chama hicho nk, ni wazi kuwa CHADEMA inahitaji mtu anayeweza kusimama kidete dhidi ya nguvu ya watawala (CCM na serikali yake) na kuhakikisha anaongoza harakati za mageuzi ya kweli

Amesema licha ya kwamba anatambua kazi kubwa iliyofanywa na Freeman Mbowe katika kipindi chote cha takribani miaka 21 aliyoongoza chama hicho kama Mwenyekiti wa Taifa, lakini yeye mwenyewe (Mbowe) ni vyema angetumia busara zake kutochukua fomu ya kuwania nafasi hiyo tena ili kutoa nafasi kwa Tundu Lissu ambaye kwa mujibu wa Bob anaamini kwamba ni turufu nzuri kwa chama hicho kuelekea kwenye mageuzi wanayoyapigia kelele kwa muda mrefu

Kuhusu madai yanayoeleza kuwa endapo Lissu atachaguliwa kuongoza chama hicho basi hakitakuwa salama kutokana na misimamo yake ambayo kwa namna moja au nyingine inaweza kuathiri taasisi kwa kuwa hana busara, Bob anasema madai hayo sio ya msingi na kwamba ni vyema yakipuuzwa kwa kuwa hata sasa chama hicho hakiko salama

“Mpaka sasa hivi chama hakiko salama, kwa maana ya usalama ambao tunauzungumzia nathubutu kusema chama hakiko salama, ndio maana hadi sasa unaona watu wanakamatwa, wanatekwa, wanauawa, na mbaya zaidi tunaelezwa kwamba sasa hivi kuna harufu hadi za rushwa kwa baadhi ya viongozi, lakini pia kumekuwa na shida kwenye sekretarieti ya chama kwamba taarifa za siri zinavuja sana, kwa hiyo kwa mazingira haya tunayoyazungumzia kama tunamkataa Lissu kwa sababu eti chama hakiko salama nadhani sio sahihi” -Bob

Aidha, Bob Chacha Wangwe ambaye pia ni Mkurugenzi mtendaji wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) ameieleza Jambo TV kuwa amesema kwa sasa Lissu ana kila sababu ya kutilia shaka uhuru na uwazi wa uchaguzi huo wa ndani ya chama kwa kuwa kwa kiasi kikubwa hana imani na maafisa waandamizi wanaoratibu uchaguzi huo ambao kimsingi ni wajumbe wa sekretarieti ya CHADEMA ndio maana hivi karibuni ameshauri kwamba viongozi wa Dini na Wanadiplomasia waalikwe kwenye mkutano mkuu ili washuhudie mambo yanavyoenda, hata hivyo anaamini kwamba atashinda uchaguzi huo

“Lissu atashinda uchaguzi, sio vizuri sana kuisema hii mapema lakini unaweza ukaona tu aina ya watu wanaomuunga mkono utapata majibu, mimi kwa maoni yangu kwa mfano Mheshimiwa Mbowe siku ile (aliyokutana na Wahariri wa Vyombo vya Habari na Waandishi wa Habari Waandamizi) angesema nimeingoza chama hiki kwa miaka 21, na kwa sababu Tundu Lissu amejitokeza, na kwa sababu miaka yake yote hajawahi kugombea kwa kupenda, lakini kwa sasa  namuachia huyu, watu wangemuheshimu sana” -Bob

Katika hatua nyingine, Bob ametoa wito kwa wanachama wa CHADEMA hususani wajumbe wa mkutano mkuu kuhakikisha wanafanya maamuzi sahihi yatakayokinufaisha chama hicho, kwani kabla ya kupiga kura kwanza wanapaswa kutafakari mwenendo wa siasa na demokrasia hapa nchini sambamba na mustakabali wa chama chao na Taifa kwa ujumla kwa siku za usoni.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!