Waandishi wa habari 36 kutoka mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Kagera, na Geita wamekutana jijini Mwanza katika mafunzo maalumu yaliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa lengo la kuwajengea uwezo na kukuza uelewa kuhusu majukumu ya benki hiyo, ili kuwawezesha kuandika kwa ufahamu zaidi katika nyanja za uchumi na fedha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Mwanza, Bi. Gloria Mwaikambo, amebainisha kuwa kwa zaidi ya miaka 12, Benki Kuu imekuwa ikikutana na waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo na kuimarisha ushirikiano.
“Tunatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika jamii yetu. Ninyi waandishi wa habari ni njia muhimu kwa Benki Kuu katika kuwafikia wananchi kupitia taarifa na makala zenu,” amesema Bi. Gloria Mwaikambo.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo unalenga kukuza maendeleo ya fedha na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Edwin Soko, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza, ameipongeza Benki Kuu kwa kutambua umuhimu wa waandishi wa habari katika kuwajengea uwezo ili kuhakikisha wanaelewa vyema masuala yanayohusu benki hiyo.
“Tunaishukuru Benki Kuu kwa kutambua umuhimu wa kutuendeleza kielimu na kutuongezea ujuzi ili tuweze kufikisha ujumbe kwa umma kwa ufanisi zaidi,” amesema Soko.
Mafunzo hayo yanalenga kuboresha uandishi wa habari za uchumi na fedha, hivyo kusaidia kuelimisha umma juu ya majukumu ya Benki Kuu ya Tanzania katika kudhibiti na kusimamia uchumi wa taifa.