Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza mshtuko wake mkubwa na kulaani vikali tukio la kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Dkt. Charles Kitima, lililotokea usiku wa Aprili 30, 2025, katika eneo la Kurasini, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa, Padre Kitima amevamiwa na watu wawili wasiojulikana na kushambuliwa kwa kutumia kitu butu kichwani na mwilini, hali iliyosababisha majeraha na kulazwa hospitalini.
“Kitendo hiki ni cha kikatili, hakikubaliki katika jamii yoyote inayojali utu na heshima ya binadamu, hasa kwa viongozi wa dini ambao wamejitolea kuhudumia watu kwa uadilifu,” amesema Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kupitia taarifa kwa umma.
CCM imeungana na kauli ya awali ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Mzee Stephen Wasira, kulaani vikali tukio hilo, na kuwataka wahusika wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo.
“Tunatoa wito kwa vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina, wa haraka, na kwa uwazi ili haki itendeke kwa Padre Kitima, familia yake na jamii kwa ujumla,” ameongeza Balozi Dkt. Nchimbi.
Chama pia kimetoa pole kwa Padre Kitima, familia yake, Baraza la Maaskofu Katoliki na waumini wote wa Kanisa Katoliki kwa mshtuko na maumivu yaliyoletwa na tukio hilo.
“Tunamuombea Padre Kitima uponaji wa haraka na kurejea salama katika majukumu yake ya kiroho na kijamii,” amesema Katibu Mkuu huyo.
CCM imerejea msimamo wake wa kuendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kulinda misingi ya amani, haki za binadamu na mshikamano wa kitaifa.