Latest Posts

DC BOMBOKO ATOA SIKU 7 MADARASA NA MABWENI KUKAMILIKA

Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Hassan Bomboko ametoa siku saba kwa wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa madarasa katika shule za sekondari Hai Day na Saashisha zilizopo kata ya Muungano kumaliza kwa wakati na kukabidhi kwa serikali ili wanafunzi waanze kutumia madarasa na mabweni.

Ametoa maagizo hayo Februari 24, 2025 katika mwanzo wa ziara yake wilayani humo yenye lengo la kuimarisha huduma za kijamii kwa umma, kusikiliza na kutatua kero za wananchi, ukaguzi wa miradi ya maendeleo pamoja na utoaji wa elimu kwa umma katika masuala ya ulipaji wa kodi na ushuru wa serikali.

“Miradi hii ilipaswa kukabidhiwa kwa Serikali Februari 16,2025 ila mpaka sasa bado japo ipo katika hatua nzuri ya ukamilishaji wa mambo madogomadogo, hivyo ninatoa siku saba ujenzi wa madarasa na mabweni uwe umekamilika na huduma zote zianze kutumiwa na wanafunzi”, ameeleza Bomboko.

Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Muungano, Edmund Rutaraka amemuomba Mkuu huyo wa Wilaya kusaidia shule ya Hai Day kupata uzio ili wanafunzi wawe katika mazingira bora kutokana na shule hiyo kuwa ya kutwa na bweni.

Jumla ya shilingi milioni 479 zinatumika katika ujenzi wa mabweni mawili na vyumba vinne vya madarasa, matundu 10 ya vyoo vya wanafunzi na nyumba ya watumishi katika Shule ya Sekondari Saashisha huku milioni 520 zikitumika katika ujenzi wa mabweni manne katika shule ya Sekondari Hai Day kutoka katika mradi wa Sequip na EP4R.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!