Latest Posts

DC BUHIGWE AWATAKA BODABODA KUFICHUA UHALIFU, NI BAADA KUHITIMU UDEREVA VETA

Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) wilayani Buhigwe, mkoani Kigoma, kimehitimisha mafunzo kwa madereva bodaboda 153, madereva wa magari 17, na wanafunzi watatu wa kozi za ujenzi, fundi bomba, na kompyuta, ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake.

Mkuu wa Chuo cha VETA Buhigwe, Ally Bushiri, alieleza mafanikio hayo katika mahafali ya kwanza ya chuo hicho, akibainisha kuwa kozi mbalimbali zimeendelea kutolewa, zikiwemo za muda mfupi na mrefu kama vile ufundi seremala, uchomeleaji, ujenzi, cherehani, na udereva wa magari ya abiria.

Bushiri alitaja changamoto ya mwitikio mdogo wa wanabuhigwe kujiunga na chuo hicho, huku akisema juhudi za kuhamasisha jamii zinaendelea ili kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka wilaya hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanal Michael Ngayalina, kupitia hotuba iliyowasilishwa na Afisa Tawala wa Wilaya, Emma Malilo, aliwataka madereva bodaboda wilayani humo kufichua wahalifu na vitendo vya kihalifu vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii.

“Wakati mwingine unapombeba mtu unajua kabisa anakwenda kuvamia sehemu fulani, lakini unaamua kunyamaza. Natoa wito kwa madereva wote kutoa taarifa wanapohisi kuna tishio, kwa usalama wao na wa jamii,” alisema Kanal Ngayalina.

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya aliwasihi madereva hao kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani ili kulinda usalama wao na wa abiria wao.

Afisa Tawala, Emma Malilo, aliwahimiza wakazi wa Buhigwe kutumia Chuo cha VETA kusomesha watoto wao, akisema chuo hicho kilianzishwa ili kusogeza huduma karibu na jamii.

“Takwimu zinaonyesha kwamba kati ya wanafunzi 86 wa VETA Buhigwe, ni wanafunzi sita tu wanaotoka wilayani hapa, hali inayohitaji kufanyiwa kazi. Tunapaswa kuwa mabalozi wa chuo hiki ili vijana wengi zaidi wapate elimu ya ufundi hapa,” alisema.

Chuo cha VETA Buhigwe kimejengwa na serikali kwa lengo la kusaidia vijana kupata ujuzi wa ufundi stadi na kupunguza changamoto ya kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya elimu hiyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!