Latest Posts

DC MPOGOLO AAGIZA KUSITISHWA KWA UJENZI WA UKUTA ULIOZIBA BARABARA KARAKATA

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameagiza kufutwa mara moja kwa kibali cha ujenzi wa ukuta unaozua mgogoro katika Mtaa wa Karakata, Kata ya Kipawa, baada ya kubainika kuwa ujenzi huo umefunga barabara inayotumiwa na wananchi kwa miaka mingi.

Mpogolo alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kukagua eneo hilo lililoko jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ambapo wananchi walieleza kukerwa na hatua ya mwekezaji huyo kuziba njia ya umma na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi.

“Namtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji kufuta kibali hicho mara moja, na kuzuia ujenzi wowote unaoziba barabara hadi muafaka wa mgogoro huu utakapopatikana,” alisema Mpogolo mbele ya wananchi waliojitokeza kwa wingi.

Mkuu huyo wa Wilaya pia alieleza kuwa atashirikiana na Mkurugenzi wa Jiji kufuatilia nyaraka zote za upimaji wa eneo hilo, hususan mchakato wa upatikanaji wa hati na uhalali wa mipango miji iliyofanyika.

“Tutapitia nyaraka zote, kuanzia hati hadi upimaji wa eneo hili. Tutaelekeza mamlaka nyingine kuchukua hatua iwapo kutakuwa na dosari au uvunjifu wa sheria,” alisema Mpogolo.

Aidha, alisisitiza kuwa dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuona wananchi wake wanaishi kwa amani na haki, hivyo viongozi wa serikali wanapaswa kuwa sehemu ya suluhisho, si chanzo cha migogoro.

“Rais wetu anataka tuishi na shida za wananchi. Lazima tuwasikilize, tuwe sehemu ya kutatua migogoro, si kuibua matatizo mapya kwa kuidhinisha miradi inayowaumiza wananchi,” alisema.

Wakazi wa Kata ya Kipawa walilipuka kwa shangwe mara baada ya Mpogolo kutoa agizo hilo, wakieleza kuwa wamekuwa wakikumbana na usumbufu mkubwa kutokana na kufungwa kwa barabara hiyo ya muda mrefu.

Hata hivyo, mmoja wa maofisa wa Halmashauri ya Jiji alieleza kuwa eneo hilo lilipimwa rasmi na lina hati, lakini hoja hiyo ilipingwa vikali na wananchi ambao walisisitiza kuwa eneo hilo lilikuwa linamilikiwa kijamii kwa miongo kadhaa bila mipango ya upimaji inayojumuisha njia za umma.

Mpogolo alihitimisha kwa kuelekeza kuwa hadi pale muafaka utakapopatikana, njia hiyo ibaki wazi kwa matumizi ya wananchi kama ilivyokuwa awali.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!