Latest Posts

DC MPOGOLO APOKEA TAARIFA UBORESHAJI SHULE ZA MSINGI OLYMPIO DIAMOND, ZANAKI BUNGE, MZIZIMA NA KISUTU

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amepokea taarifa maalum ya mikakati ya uboreshaji wa Shule za Msingi Olympio, Diamond, Zanaki, Bunge, Mzizima, na Kisutu, yenye lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi kwa mwaka 2025 na kuinua kiwango cha taaluma.

Akizungumza siku ya Alhamisi Januari 9, 2025 baada ya kupokea taarifa hiyo, Mpogolo amesema hatua hizo zinalenga kuboresha mazingira ya utoaji elimu na kuhakikisha shule hizo zinakidhi viwango vya kusomea na kufundishia, sambamba na kukuza ufaulu wa wanafunzi.

Mpogolo ameongeza kuwa mpango huo umejikita zaidi katika kupunguza idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kujiunga na darasa la kwanza kwa mwaka huu wa 2025.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, idadi ya wanafunzi walioandikishwa kwenye shule mbalimbali ni kama ifuatavyo: Shule ya Msingi Bunge imeandikisha wavulana 150 na wasichana 136, jumla 286; Shule ya Msingi Zanaki imeandikisha wavulana 153 na wasichana 175, jumla 328; Shule ya Msingi Kisutu imeandikisha wavulana 138 na wasichana 136, jumla 274; na Shule ya Msingi Mzizima imeandikisha wavulana 102 na wasichana 108, jumla 210. Jumla ya wanafunzi walioandikishwa katika shule hizo kwa mwaka 2025 ni 1,211.

Awali, Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Macha Manase, amesema kuwa kwa Shule ya Msingi Diamond, jumla ya wanafunzi walioandikishwa kwa mwaka huu ni 255, wakiwemo wavulana 131 na wasichana 125.

Aidha, ameeleza kuwa mwaka jana 2024, idadi ya wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi katika shule hiyo ilikuwa wavulana 280 na wasichana 242, jumla 522, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na mwaka huu.

Kwa upande wa Shule ya Msingi Olympio, wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi mwaka 2024 walikuwa wavulana 395 na wasichana 390, jumla 785, huku mwaka huu shule hiyo ikiwa imeandikisha jumla ya wanafunzi 500, wakiwemo wavulana 240 na wasichana 260. Mpango huu wa kupunguza msongamano na kuboresha taaluma unaendana na dhamira ya serikali ya kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!