Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeweka dhamira ya kuhakikisha usawa wa kijinsia katika udahili kwa kutoa kipaumbele kwa wasichana wanaotaka kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi. Azma hiyo inalenga kufanikisha shabaha ya kufikia asilimia 50 ya udahili wa wasichana katika vyuo vya VETA.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, tarehe 19 Novemba 2024, wakati wa kuhitimisha uchaguzi wa wanafunzi walioomba kujiunga na vyuo vya VETA kwa mwaka wa masomo wa Januari 2025. Tukio hilo limefanyika katika Chuo cha VETA Dodoma na kuhudhuriwa na wasajili kutoka vyuo vyote vya VETA nchini.
CPA Kasore amesisitiza kuwa juhudi hizi zinalenga kuongeza mwamko wa wasichana na wanawake kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi, hasa kwenye fani ambazo kwa sasa zimejaa wanafunzi wa kiume.
“Mathalani, fani za Uashi, Uundaji na Uungaji Vyuma, Undeshaji Mitambo Mikubwa, na Ufundi Magari, bado hazina uwakilishi mzuri wa wasichana. Tunahitaji kuweka msukumo ili kubadilisha hali hiyo,” amesema Kasore.
Ameongeza kuwa mafanikio ya wahitimu wa kike katika sekta za ufundi yameanza kuleta hamasa, na kwa kuhakikisha udahili wa wasichana unaongezeka, mafanikio hayo yatakuwa mfano bora wa kuigwa na wengine.
Katika kikao hicho cha siku mbili, wasajili wa vyuo vya VETA walijengewa uwezo wa kudahili wanafunzi kwa kutumia mfumo wa kidijiti, huku wasajili wapya wakipata mafunzo ya kuingiza takwimu na taarifa za wanafunzi wapya kwenye mfumo.
Mkurugenzi wa Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA, Dkt. Abdallah Ngodu, amesema kikao hicho pia kililenga kufanya msawazo wa wanafunzi kwenye vyuo vya VETA ili kuweka uwiano mzuri wa udahili katika vyuo vyote nchini.