Latest Posts

FENSI YA UMEME GRUMETI FUND YATAJWA KAMA SULUHISHO LA KUZUIA TEMBO

Fensi ya umeme ya majaribio iliyowekwa na shirika lisilo la kiserikali la Grumeti Fund katika vijiji vinavyozunguka Mapori ya Akiba ya Ikorongo na Grumeti imetajwa kusaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, hasa tembo. Hali hiyo imewafanya wadau wa uhifadhi na utalii kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kueneza teknolojia hiyo kwenye maeneo mengine yenye changamoto kama hizo.

Wadau hao wametoa maoni yao baada ya kutembelea eneo lenye fensi hiyo katika wilaya ya Serengeti mkoani Mara na kujionea jinsi ambavyo imepunguza mwingiliano wa wanyama hatari, kupunguza uharibifu wa mazao, na kulinda maisha ya binadamu.

Noel Mbise, Meneja Mkuu wa Utafiti na Jamii kutoka Grumeti Fund, amesema fensi hiyo yenye urefu wa takriban kilomita 30 katika maeneo ya Park Nyigoti, Miseke na vijiji vya jirani, imeleta manufaa makubwa kwa usalama wa wanavijiji na wanyama.

“Malalamiko kutoka kwa wananchi yamepungua. Tembo anapogusa fensi, hupata mshtuko mdogo wa umeme na kurudi porini. Hii imesaidia kuweka mipaka salama kati ya makazi ya watu na hifadhi,” alisema Mbise.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato, Bw. Ombeni Higi, amesema wamevutiwa na teknolojia hiyo na wanaamini kwamba ikitumiwa vizuri katika maeneo kama Burigi ambako tembo husababisha migogoro mingi, itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto hizo.

Michael Kimaro, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Tanzania Research and Conservation (TRC), alisema lengo la kuanzisha fensi hiyo lilikuwa kufanya majaribio ya kuona namna ya kusaidia jamii dhidi ya madhara yatokanayo na wanyama, na sasa matokeo yake ni chanya.

“Tunaomba serikali iangalie namna ya kufadhili au kushirikiana na taasisi hizi ili kupanua mfumo huu hadi maeneo mengine yenye migogoro. Hii ni hatua bora ya kuzuia majeraha, vifo na uharibifu wa mali za wananchi.”

Kwa sasa, wadau wanasisitiza kuwa teknolojia kama hii si tu inalinda maisha, bali pia inasaidia kuhifadhi wanyamapori kwa njia inayozingatia haki na usalama wa binadamu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!