Latest Posts

GACHAGUA ASEMA POLISI WALIJARIBU KUMUUA KWA SUMU MARA MBILI

Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, amedai kuwa alinusurika majaribio mawili ya kuuawa kwa sumu kabla ya hoja ya kumwondoa madarakani kuwasilishwa Bungeni.

Gachagua amezungumza na wanahabari baada ya kuondoka hospitali ya Karen, Nairobi, ambako alikuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua wiki iliyopita.

“Sijisikii salama,” amesema Gachagua. “Mnamo Agosti 30, maafisa wa polisi wa siri huko Kisumu walivamia chumba changu na mmoja wao akajaribu kutia sumu kwenye chakula changu, lakini tuligundua na tukaweza kutoroka. Nililenga kuuawa kwa sumu.”

Ameendelea kueleza kuwa tukio jingine lilitokea Septemba 3, katika eneo la Nyeri, ambapo maafisa wa Huduma ya Ujasusi ya Kitaifa (NIS) walijaribu tena kumtilia sumu kupitia chakula kilichokuwa kimetayarishwa kwa ajili yake na wazee wa Kikuyu.

Gachagua amedai kuwa aliripoti suala hilo kwa NIS na kuwataka maafisa waliokuwa wamepangiwa ofisi yake kuondoka.

Gachagua ameeleza kuwa baada ya njama za kumuua kushindikana, hatua ya pili ilikuwa kuanzisha hoja ya kumwondoa madarakani. Amesema kuwa mashtaka ya kumwondoa yamekuja kutokana na msimamo wake dhidi ya baadhi ya maamuzi ya serikali, ikiwemo suala la kuondoa watu kutoka kwenye ardhi ya mto Nairobi na mpango wa kukodisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kampuni ya Adani kutoka India.

Katika mazungumzo hayo, Rigathi Gachagua amemshutumu Rais William Ruto kwa kumkandamiza na kumsaliti, akidai kuwa walikuwa na makubaliano ya ushirikiano kabla ya kuchukua madaraka mwaka 2022.

“Nilimwamini Rais William Ruto, watu wa Mlima Kenya walimwamini. Tulipokuwa tukijiandaa kwenda ofisini, hakuna mtu mwingine aliyemwamini. Mimi ndiye niliyemwamini kwa sababu sisi ni Wakristo. Tulikuwa tukienda kanisani pamoja. Niliamini Mkristo mwenzangu, kwamba hatawahi kunisaliti mimi au watu wangu,” amesema Gachagua.

Aliendelea kueleza kuwa anashtakiwa kwa sababu ya kusema ukweli kuhusu mambo mbalimbali serikalini, akiwemo msimamo wake kuhusu masuala nyeti kama uhamishaji wa watu kwenye ardhi za serikali na mikataba ya serikali na mashirika ya kigeni.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!