Serikali imeombwa kufikiria upya mfumo wa kodi unaozikabili hospitali zinazomilikiwa na taasisi za dini, ili kurahisisha uendeshaji wa huduma hizo ambazo zimeanzishwa kwa dhamira ya kutoa msaada kwa wananchi na si kwa lengo la kibiashara.
Wito huo umetolewa na Padre Inocent Chaula, Katibu wa Afya na Katibu wa Mhashamu Askofu Ausebius Kyando wa Jimbo Katoliki la Njombe, wakati wa maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Ukristo ya mwaka 2025 yaliyofanyika katika Hospitali ya St. Joseph Ikelu, iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Makambako.
“Hospitali hizi zimeanzishwa kwa lengo la kutimiza wajibu wa kanisa wa kuhudumia mtu kimwili na kiroho. Changamoto ya kodi na bima zinatufanya tuendeshe huduma kwa shida. Tuwaombe viongozi wetu wa serikali waliopo watusemee,” alisema Padre Chaula mbele ya waumini, viongozi wa serikali na wananchi waliohudhuria tukio hilo.
Amesema licha ya hospitali hizo kuwa chini ya taasisi binafsi, huduma zake nyingi ni za kijamii na mara nyingi hazina faida yoyote, bali hutoa msaada kwa watu wenye uhitaji mkubwa, hususan maeneo ya vijijini ambako serikali haijafika kwa haraka.
Aidha, ameeleza changamoto zinazotokana na mifumo ya bima ya afya, ambayo imekuwa ikiwabana watoa huduma kwa vifurushi visivyokidhi gharama halisi za huduma wanazotoa kwa wagonjwa.
“Katika miaka ya karibuni, sekta binafsi ya kidini imekuwa ikihisi ukali wa mifumo ya kodi na bima. Tunaiomba serikali ione tofauti ya biashara na huduma za huruma kwa jamii,” ameongeza.
Katika maadhimisho hayo, Padre Chaula pia amewataka wahudumu wa afya kuwa watu wa matumaini na faraja kwa wagonjwa, na akaipongeza hospitali ya St. Joseph Ikelu kwa kutoa huduma ya bure ya uchunguzi wa afya kwa wananchi 412, katika siku mbili mfululizo, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Jubilei hiyo.