Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeipongeza Wizara ya Maji kwa utekelezaji wa maagizo mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa kwa Wizara.
Pongezi hizo zimetolewa jijini Dodoma baada ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuwasilisha taarifa ya Wizara kwa Kamati.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Jackson Kiswaga amesema wizara ya Maji imepiga hatua kubwa katika utatuzi wa changamoto mbalimbali katika sekta hali ambayo imewezesha changamoto za muda mrefu za sekta kupungua na zingine kuisha kabisa.
Amesema kamati inajivunia hatua hiyo na kuwataka wizara kuendelea kusimamia malengo ya msingi ambayo ni kutatua changamoto za sekta na kuhakikisha lengo la ilani ya uchaguzi linafikiwa.
Awali akiwasilisha taarifa ya wizara waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema moja ya maagizo ilikuwa ni pamoja na kuhakikisha kiwango cha upotevu wa maji kinapungua ambapo Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini zimepunguza upotevu wa maji kutoka wastani wa asilimia 36.2 kwa mwaka wa fedha 2023/24 hadi kufikia wastani wa asilimia 33.43 kwa mwezi Desemba 2024.
Amesema kupungua kwa kiwango cha upotevu wa maji katika mamlaka hizo kumechangiwa na kukamilika kwa baadhi ya miradi ya ukarabati wa miundombinu chakavu pamoja na kudhibiti wizi wa maji.
Muongozo wa Usanifu na Usimamizi wa Miradi ya Maji nchini wa Mwaka 2020 ambao unaelekeza ni lazima kuhusisha jamii pamoja na Taasisi katika maeneo husika kuanzia kuibua, kupanga, kutekeleza, kusimamia, kufuatilia na kutoa huduma ya maji.