Kamati iliyoundwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo kuchunguza wafanyabiashara wa kigeni maeneo ya Kariakoo imefikia asilimia 50 ya uchunguzi wake na imeahidi kukabidhi ripoti hiyo Machi 2, 2025 kama ilivyoagizwa.
Februari 2, 2025 Waziri Jafo aliunda Kamati ya watu 15 kuchunguza wafanyabiashara wa kigeni eneo la Kariakoo inayoongozwa na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Edda Lwoga.
Aliunda Kamati hiyo baada ya agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Januari 30, 2025, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya chakula cha mchana alichokiandaa kwa ajili ya washiriki wa shughuli ya uokoaji wa kuporomoka kwa jengo Kariakoo.
Akizungumza mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Edda Lwoga ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam (CBE) amesema baada tu ya uteuzi walianza rasmi kazi ya kuwahoji wafanyabiashara wa makundi mbalimbali kama machinga, wauza vifaa vya umeme, vifaa vya magari, vipodozi na biashara zingine.
“Hata leo hapa tuko na wafanyabiashara wa Kariakoo tunaendelea kuhojiana nao kupata taarifa zaidi kuhusu changamoto ya wafanyabiashara wa kigeni ili tuweze kutoa mapendekezo ya nini kifanyike kuondoa changamoto hii,” amesema Profesa Lwoga na kuongeza,
“Tuliagizwa tutoe ripoti yetu ndani ya siku 30 na kwa hatua ya asilimia 50 tuliyofikia tuna imani tutaikamilisha na kuikabidhi kwa mamlaka ndani ya muda huo tuliopewa”.
Amesema mbali na kukutana na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara wametoa namba ya simu ya bure ambayo mwananchi yeyote anaweza kupiga na kutoa maoni yake, namba hiyo ni 080011616 huku kwa upande wa WhatsApp namba ikiwa ni 0738 816 113.
“Tunapokea maoni kwa njia mbalimbali ili tutakapotoa ripoti iwe imegusa maeneo mbalimbali kwa hiyo mwananchi popote alipo Tanzania atoe maoni kwa hiyo tunaomba watu watupe maoni yao,” amesema.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Conrad Millinga kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu amesema lengo la kamati hiyo ni kuona kwamba biashara zinazofanyika nchini zinawanufaisha zaidi Watanzania.

“Wageni wanakaribishwa kufanya biashara nchini, huwezi kukataa wafanyabiashara wa kigeni lakini tunataka wakija wafanye biashara zao kwa kufuata kanuni na taratibu za nchi zilizopo wasifanye kiholela tu,” amesema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severini Mushi amewaomba wafanyabiashara kuitumia kikamilifu fursa hiyo waliyoipata kutoka serikalini kutoa maoni yao ili changamoto hiyo iweze kupatiwa ufumbuzi.
“Njooni mtoe ushirikiano kwa kamati ambayo imetembelea wafanyabiashara mbalimbali na tukitoa ushirikiano wa kutosha kwa kamati hii tutaiwezesha kumaliza kazi yake kwa wakati na kutoa ripoti yake kwa Waziri,” amesema.
Mjumbe mwingine kutoka kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ted Sikuluwasha amesema mbali na kukutana na wafanyabiashara, kamati itafanya mahojiano na baadhi ya taasisi za serikali kuhusu changamoto hiyo.
Amesema kamati hiyo itafanya kazi zake kwa umakini mkubwa na kuishauri serikali namna bora ya kuondoa changemoto hiyo ili kuweka ushindani ulio sawa wa biashara baina ya wageni na Watanzania.
“Tunapambana kuikamikilisha hii kazi kwa wakati lakini lazima tuzifikie pande zote ili tuweze kushauri vizuri kwenye ripoti tutakayoandaa, tumefikia asilimia 50 na tunaamini Machi 2 tutakabidhi ripoti,” amesema.