Latest Posts

KAMPUNI ZA MADINI ZAZALISHA AJIRA 19,356 WAZAWA 18,853

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Wizara hiyo imeendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kuzalisha ajira zaidi kwa Watanzania kutoka kwenye kampuni mbalimbali za uchimbaji madini ambapo katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2023 kampuni za uchimbaji madini ziliweza kuzalisha ajira 19,356 na kati ya hizo ajira 18,853 sawa na asilimia 97.40 ni Watanzania.

Mavunde amebainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita Alhamisi Mei 15, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.

Amesema katika kipindi hicho jumla ya bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.9 ziliuzwa na kusambazwa migodini ambapo kati ya hizo Kampuni za Watanzania zilifanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.5 sawa na asilimia 92 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote na huduma zilizotolewa migodini.

“Mchango wa Sekta ya Madini katika fedha za kigeni kwa mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi umeendelea kuimarika kutoka Dola za Marekani bilioni 3.1 sawa na asilimia 45.9 mwaka 2021 hadi Dola za Marekani bilioni 3.55 sawa na asilimia 46.1 mwaka 2023,” ameeleza na kuongeza.

“Pia, kwa upande wa mauzo ya bidhaa zisizo asilia (non-traditional goods), mchango wa sekta ya madini umeongezeka kutoka asilimia 53.8 mwaka 2021 hadi asilimia 56.2 mwaka 2023,” Amefafanua Waziri Mavunde.

Aidha, ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa masoko ya madini mwaka 2019, Masoko na Vituo vya Ununuzi vimeongezeka kutoka 42 na 100 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 43 na 109 mwaka 2024/2025 mtawalia na katika mwaka wa fedha 2024/2025, wizara imeyatambua na kuyapa hadhi ya vituo vya ununuzi jumla ya maeneo 142 yanayotumika kufanyia biashara ya madini kwa wingi (bulk minerals) kupitia Gazeti la Serikali Na. 906 ya tarehe 15 Novemba, 2024.

Hata hivyo Waziri Mavunde amesema serikali ya awamu ya sita kupitia tume ya madini imekuwa ikitoa leseni za uendeshaji wa shughuli za madini kwa wadau wake kwa kuzingatia Sheria ya Madini, Sura 123 na katika kipindi cha kuanzia 2021/2022 hadi Mei, 2025 tume ya Madini imetoa jumla ya leseni 34,348 ikijumuisha leseni za Uchimbaji Mkubwa, Uchimbaji wa Kati, Uchimbaji Mdogo, biashara ya madini pamoja na uchenjuaji wa madini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!