Baadhi ya wananchi wa Kata ya Chibe, Manispaa ya Shinyanga, wameonyesha furaha yao juu ya ujenzi wa daraja jipya linalowaunganisha kwenye shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Hata hivyo, wameeleza wasiwasi wao kuhusu ukosefu wa taa eneo hilo, hali inayohatarisha usalama hasa nyakati za usiku.
Wakizungumza Februari 20, 2025, wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Wazazi Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mlindoko, wananchi hao wamesema daraja hilo limekuwa mkombozi kwao kwani awali walikuwa wanapata changamoto kubwa ya kuvuka hasa wakati wa mvua.
Mkazi wa kata hiyo, Benadetha Edward, amesema kuwa daraja hilo litarahisisha shughuli zao za kilimo na biashara kwani awali walikuwa wanashindwa kuvuka kwenda shambani au mnadani.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Chibe, John Kisandu, amesema barabara hiyo ilikuwa ya kikoloni na baada ya kufanyiwa ukarabati na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), imeleta mafanikio makubwa kwa kuwaunganisha wafanyabiashara wa mikoa ya Tabora, Shinyanga, na Mwanza.
Ameongeza kuwa kabla ya ujenzi wa daraja hilo, mvua ziliponyesha walikuwa wanapata shida kuvuka, lakini sasa linaweza kusaidia kuongeza mapato ya Manispaa. Hata hivyo, ameiomba serikali kuweka taa za barabarani katika eneo hilo ili kuimarisha usalama wa wakazi na wasafiri wanaopitia hapo nyakati za usiku.
Mwenyekiti wa Wazazi Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mlindoko, amepongeza ujenzi wa daraja hilo na kuahidi kufikisha ombi la wananchi kwa mamlaka husika kuhusu uwekaji wa taa ili kuhakikisha usalama wa wananchi nyakati za usiku.