Katibu Mkuu wa Umoja wa Walimu Wasio na Ajira Tanzania (NETO), Daniel Edigar Mkinga, amedaiwa kukamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani akiwa nyumbani kwake Kibaha, Miembe Saba majira ya saa tatu kasoro usiku wa siku ya Jumanne Februari 25, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa alizotoa mke wake, Mkinga alikamatwa na askari watatu kutoka kituo cha Polisi Maili Moja Kibaha, katika ushuhuda wa viongozi wa mtaa wake akiwemo Balozi na Mjumbe.
Taarifa iliyotolewa na NETO tarehe 25 Februari 2025, inaeleza kuwa Mkinga anashikiliwa kwa tuhuma zinazohusiana na ushiriki wake katika jumuiya hiyo. Agness Mpundi, Makamu Mwenyekiti wa NETO, ametoa wito kwa wanasheria na mashirika ya haki za binadamu kusaidia kuhakikisha Mkinga anapata uhuru wake.
“Tunaendelea kuwakumbusha kuwa NETO si chama cha siasa, wala haina nia yoyote ovu dhidi ya amani ya nchi yetu. Umoja huu unahimiza serikali kutoa ajira kwa walimu na kutekeleza makala tulizoandika kwa mamlaka husika,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo, huku NETO ikisisitiza kuwa itaendelea kupigania haki ya walimu wasio na ajira na kuomba serikali ifanyie kazi madai yao.
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umelaani vikali kukamatwa kwa Mkinga ikieleza kuwa imechukua hatua za kisheria kwa kumtuma wakili wake kufuatilia dhamana ya Mkinga na imelitaka Jeshi la Polisi kumuachia mara moja, kwani hakuna kosa lolote alilotenda kwa kudai haki za walimu, hata hivyo juhudi za kupata kauli ya polisi juu ya kukamatwa kwa Mkinga bado zinaendelea.
“Hatutaacha kufuatilia suala hili kuhakikisha kuwa Katibu wa NETO anapata haki zake kwa mujibu wa sheria,” imeeleza THRDC katika tamko lake rasmi.
Madai ya kukamatwa kwa Katibu Mkuu NETO yanakuja saaa chache baada ya Jeshi la Polisi mkoa wa Geita kukiri kumshikilia Joseph Paul (31), Mwenyekiti wa NETO kwa ajili ya mahojiano kutokana na madai ya kuhusika na kundi hilo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita SACP Safia Jongo, Paul alikamatwa Februari 24, 2025, baada ya uchunguzi wa awali kubaini kuwa umoja huo hauna usajili rasmi kutoka kwa mamlaka husika.
Polisi walisema mtuhumiwa alihojiwa kwa mujibu wa sheria, kuelezwa tuhuma dhidi yake, na kwa sasa yuko nje kwa dhamana huku uchunguzi ukiendelea.