Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amemshutumu mwanasiasa wa Kenya Martha Karua kwa kile alichokiita uchochezi na uvunjaji wa kanuni za uangalizi wa haki za binadamu, akidai kuwa kiongozi huyo alitumia vibaya nafasi yake kwa kutoa matamko yenye kuibua chuki na uhasama dhidi ya Serikali ya Tanzania.
Akizungumza katika mahojiano maalum na BBC Swahili usiku wa Jumatano Mei 21, 2025, Wasira alisema Karua alivuka mipaka ya kiutaratibu alipokuja nchini na kutoa kauli za kisiasa akiwa mbele ya Mahakama ya Kisutu, badala ya kuzingatia wajibu wa mgeni na mwangalizi.
“Mtu ambaye amewaponza wenzake ni Martha Karua, maana alipokuja mara ya kwanza aliingia nchini, akaenda Kisutu na akasema amekuja kwa kofia mbili — kama mwanasheria na kama mwanasiasa wa Kenya mwenye chama chake cha Peoples Liberation Party,” alisema Wasira.
Kwa mujibu wa Wasira, Karua alienda mbali zaidi kwa kudai kuwa kukamatwa kwa Tundu Lissu ni ushahidi kwamba Serikali ya Tanzania inaogopa CHADEMA, na kutaka Lissu aachiwe huru bila masharti pamoja na kuiruhusu CHADEMA kushiriki uchaguzi. Kauli hizo, kwa mujibu wa Wasira, zilikiuka misingi ya uangalizi huru wa haki za binadamu.
“Kama observer wa sheria huendi na judgment, kazi yako ni kuangalia mwenendo, lakini yeye alishakuwa judgemental — ameshajua mbaya ni nani na solution ni ipi,” aliongeza.
Wasira alidai kuwa matamshi ya Karua yaliibua wasiwasi ndani ya vyombo vya dola, yakihisiwa kuwa na ajenda ya kuchochea ghasia au kuwagawa Watanzania, hali iliyopelekea hatua zaidi kuchukuliwa dhidi ya wageni wengine waliokuja wakidai kuunga mkono haki za binadamu katika kesi ya Tundu Lissu.
“Aliprovoke system… ilionekana kwamba shabaha yake sio kuwa muangalizi huru bali ni kuchochea ghasia. Kwahiyo pamoja na kwamba yeye alikuja, wengine sasa alishawachongea,” alisema Wasira.
Kauli hiyo ya Wasira inakuja siku moja tu baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, kueleza kuwa wageni kutoka Kenya waliokuja kushiriki kesi ya Lissu walikosa vibali vya kufanya kazi za kisheria nchini, hivyo kuvunja sheria.
Kesi ya Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na mashtaka mbalimbali yakiwemo ya uhaini, imeendelea kuvuta hisia za mashirika ya haki za binadamu na jumuiya ya kimataifa, huku Serikali ya Tanzania ikisisitiza kuwa haki na utawala wa sheria vinazingatiwa.