Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeeleza masikitiko yake juu ya hali ya kukosa dhamana kwa mwanadiplomasia na mwanasiasa mkongwe, Dkt. Willibrod Slaa, aliyekamatwa tarehe 9 Januari 2025 kwa tuhuma za kuchapisha taarifa za uongo, kinyume na Sheria ya Makosa ya Mtandao Na. 14 ya mwaka 2015.
Katika taarifa ya siku ya Jumatatu Januari 27, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt. Anna Henga amesema Dkt. Slaa alifikishwa siku hiyohiyo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kupitia shauri la jinai Na. 993 la mwaka 2024, ambapo, licha ya kosa hilo kutokuwa miongoni mwa makosa yasiyo na dhamana kama ilivyoanishwa katika kifungu cha 148(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 (mapitio ya 2022), Jamhuri iliwasilisha shauri dogo la kuzuia dhamana yake.
Amesisitiza kuwa dhamana ni haki ya msingi ya kikatiba, kama ilivyoainishwa katika ibara ya 13(6)(a) na 15 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, pamoja na mikataba ya kikanda na kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama wake.
“Ni muhimu kwa vyombo vya upelelezi na usimamizi wa haki kuheshimu sheria zilizopo na kutowazuia watuhumiwa kupata dhamana pale ambapo kosa linaruhusu dhamana kisheria.” Amesema, Dkt. Henga.
LHRC imetaja matukio kadhaa ya nyuma, ambapo Watanzania walikosa dhamana kinyume cha sheria, ikiwa ni pamoja na kesi ya aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, na kada wa CHADEMA mkoa wa Tanga, Kombo Mbwana. Makosa kama haya, ambayo hayajumuishwi katika kifungu cha 148(5), yanapaswa kuruhusu dhamana kulingana na sheria.
LHRC pia imekumbusha kuwa mwaka 2022, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ilifanyiwa marekebisho kwa kuongezwa kifungu cha 131A, ambacho kinapiga marufuku Jamhuri kuwasilisha kesi mahakamani kama upelelezi haujakamilika. Hata hivyo, hali kama hizi bado zinaendelea kushuhudiwa, jambo ambalo limetajwa kukiuka haki za msingi za watuhumiwa.
Katika taarifa yao, LHRC imetoa wito kwa vyombo vya upelelezi nchini kuacha utamaduni wa kuzuia dhamana kwa makosa ambayo si miongoni mwa makosa yasiyo na dhamana kwa mujibu wa kifungu cha 148(5), vyombo vya usimamizi wa haki kumpa haki ya dhamana Dkt. Wilbroad Slaa na Watanzania wengine waliokutwa na changamoto za usimamizi wa haki jinai.
“Tunatoa rai kwa mamlaka zote zinazohusika kuhakikisha kuwa haki ya dhamana ya Dkt. Slaa inaheshimiwa, na kwamba sheria inatekelezwa bila upendeleo wala kinyume na maadili ya kisheria,” amesema Dkt. Henga.