Na Amani Hamisi Mjege.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) tarehe 17 Oktoba 2024, kimezindua rasmi maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu, ambayo yataadhimishwa tarehe 10 Disemba 2024.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu “Usawa – Kupunguza Ukosefu wa Usawa na Kukuza Haki za Binadamu,” ikilenga kuongeza mwamko wa kimataifa katika kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na usawa unazingatiwa kwa wote.
Akizungumza na wanahabari kuhusu uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt. Anna Henga, amesisitiza kuwa maadhimisho haya ni kumbukizi muhimu inayozingatia Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948, lililopitishwa na Umoja wa Mataifa.
“Haki za binadamu ni msingi wa jamii yoyote iliyostaarabika, na tunapoadhimisha siku hii, ni muhimu kuzingatia changamoto zinazokabili utekelezaji wa haki hizi, hususani ukosefu wa usawa,” amesema Dkt. Henga.
LHRC imeeleza kuwa pamoja na mafanikio yaliyoafikiwa katika ulinzi wa haki za binadamu, Tanzania bado inakabiliwa na changamoto za ukiukwaji wa haki, ikiwemo vitendo vya utekaji, mauaji, na vitisho dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari. Hali hii imezua taharuki na hofu miongoni mwa wananchi, na LHRC imeitaka serikali kuweka mikakati thabiti ya kurejesha ulinzi wa haki za binadamu.
Katika kuadhimisha siku hii muhimu, LHRC imepanga matukio mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mashindano ya sanaa kwa wanafunzi wa shule za Dar es Salaam, na utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi, hususani wanawake walioathirika na matukio ya uvunjifu wa haki. Pia, LHRC itatoa elimu ya kisheria kupitia mitandao ya kijamii ili kuongeza uelewa kuhusu haki za binadamu nchini.
“Ni wajibu wetu sote kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa, na kwa mwaka huu, tumejikita zaidi katika kupambana na ukosefu wa usawa na kuhakikisha haki zinazingatiwa kwa kila mtu,” ameongeza Dkt. Henga.
Katika kilele cha maadhimisho hayo mnamo Disemba 10, LHRC itazindua mpango mkakati wake mpya wa miaka sita (2025-2030), ambao utalenga kuboresha zaidi ulinzi wa haki za binadamu nchini, sambamba na kuonyesha filamu fupi ya mafanikio ya miaka sita iliyopita katika sekta ya haki za binadamu.