Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa imetoa Mafunzo ya Siku mbili kwa Maafisa Waandikishaji Ngazi ya Kata, yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya hiyo
Lengo la Mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Maafisa Waandikishaji Ngazi ya Kata, kwa ajili ya kuboresha Daftari la kudumu la Wapiga Kura Wilayani Nyasa.
Akifungua mafunzo hayo Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Nyasa Khalid A. Khalif amewataka washiriki wa mafunzo kusikiliza mafunzo kwa makini kwa kuwa yanawajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao ili kufanikisha Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Amefafanua kuwa, Mafunzo haya yatahusisha namna ya ujazaji fomu pamoja na kutumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura, (Voters Registration System- VRS) ili waweze kupata uelewa wa pamoja na vifaa vingine vya kuandikisha Wapiga Kura hivyo basi mnatakiwa kuwa makini na kuelewa mafunzo.
“Mafunzo haya yanawajengea umahiri wa kuwafundisha Waandikishaji Wasaidizi na Waendeshaji Vifaa vya Bayometriki ambao ndio watahusika na uandikishaji wa Wapiga Kura Vituoni”. alisema Khalid
Aidha, amewaagiza Maafisa hao kuwa wakati wa Uboreshaji wa Daftari mawakala wa Vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura. Hivyo, basi mnatakiwa kuzingatia ili kuleta uwazi katika zoezi zima na kuwatambua waombaji katika maeneo yao, ila mawakala hao wasiingilie majukumu ya Watendaji.
Amewataka kutunza vifaa, kushirikiana na maafisa Ngazi ya Jimbo na kuhamasisha wananchi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili kujiandaa na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, 2025.
Alisema kuwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 12 – 18 Januari, 2025.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo wakiongozwa na Mwenyekiti wao wamesema watasikiliza mafunzo hayo kwa umakini na kufanya kazi kwa weredi.
Awali kabla ya kuanza mafunzo Mhe.Zuberi Kigwangala, Hakimu Mkazi wa mahakama ya Mwanzo Mbamba bay amewaongoza washiriki kula kiapo cha kutunza siri na kutoa Tamko la kujitoa Uanachama au kutokuwa na Mwanachama wa Chama cha Siasa