Latest Posts

MABADILIKO YA TABIANCHI YAWA KIKWAZO KWA UFUGAJI WA NYUKI KILIMANJARO NA ARUSHA

Wafugaji wa nyuki kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha wameeleza athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi kwenye ufugaji wa nyuki, hasa aina ya nyuki wasiokuwa na miiba (stingless bees), na namna hali hii inavyopunguza uzalishaji wa asali na kuhatarisha usalama wa chakula.

Barakaeli Nkini, mfugaji kutoka kijiji cha Ngarony wilayani Siha, Kilimanjaro, amesema ongezeko la joto duniani linaathiri misimu ya maua, chanzo kikuu cha chakula cha nyuki. Hali hii imewahi kumfanya ashindwe kufanikisha ufugaji katika maeneo ya KIA wilayani Hai na mjini Moshi kutokana na joto kali.

“Mabadiliko ya tabia nchi yanasababisha kuchelewa au kutokuwepo kwa misimu ya maua, jambo ambalo linapunguza uzalishaji wa asali. Hata hivyo, vijijini bado kuna chakula cha kutosha kwa nyuki kutokana na wingi wa miti, maua ya asili, na mvua za kutosha,” amesema Nkini.

Nkini pia ameongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaongeza hatari ya magonjwa na wadudu hatarishi kwa nyuki, hali inayoongeza vifo vya nyuki na kupunguza uzalishaji wa asali.

Kwa upande wake, Elinuru, maarufu kama Mama Shujaa wa Chakula 2014 kutoka Tengeru, Arusha, ameeleza kuwa nyuki wanalazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta chakula kutokana na ukataji wa miti hovyo na kilimo kisicho hifadhi mazingira. Hali hii inawaweka nyuki katika hatari ya kushambuliwa na maadui njiani.

“Mabadiliko ya mvua pia yanaathiri upatikanaji wa maua, hivyo kusababisha nyuki kupata changamoto kubwa ya chakula. Ukame unakwamisha mimea ya maua, hali inayohatarisha uzalishaji wa asali,” amesema Elinuru.

Elinuru amesisitiza umuhimu wa kilimo hai (ikolojia) ambacho ni rafiki wa mazingira, kwani husaidia kuwepo kwa chakula cha nyuki wakati wote na kuchochea uzalishaji wa mazao kupitia uchavushaji wa nyuki.

Wafugaji hawa wamehimiza mikakati endelevu ya kisasa ili kuhifadhi mazingira bora kwa ustawi wa nyuki, pamoja na juhudi za pamoja za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!