Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa baada ya maboresho yaliyofanyika kwenye sheria mbalimbali zinazosimamia uchaguzi, hakutakuwa na sababu yoyote ya kudhani kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki iwapo matokeo hayakumfurahisha mgombea au chama fulani.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika Jumanne, Aprili 29, 2025, eneo la Mwananyamala, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, amesema kuwa chama hicho kinaamini kila mshindi wa kweli atatambuliwa bila upendeleo kutokana na mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika sheria muhimu za uchaguzi.
“CCM inaamini kuwa kwa kuwa na maboresho yote yaliyofanyika kwenye sheria ya uchaguzi wa madiwani, wabunge na rais; sheria ya vyama vya siasa; na sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), basi tunaamini atakayeshinda kwa haki atangazwe kuwa mshindi,” amesema Makalla.
Akiendelea kuelezea mtazamo wa CCM kuhusu dhana ya uchaguzi huru, Makalla amewakosoa baadhi ya wanasiasa wa upinzani ambao, kwa mujibu wake, huamini uchaguzi ni huru tu pale ambapo chama tawala kimepoteza.
“Ni kama mechi ya mpira; ukishinda unasema refa alikuwa fair, lakini ukishindwa unasema palikuwa na faulo au tuta refa kaacha… hivyo hivyo uchaguzi, tunasema atakayeshinda kwa haki, atangazwe mshindi. Hiyo ndiyo ahadi yetu.”
Aidha, Makalla amesema kuwa CCM inaamini imefanya kazi kubwa ya maendeleo na kwamba kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu zitajikita katika kuuza ilani yake kwa wananchi kwa hoja na ushahidi wa utekelezaji, si malumbano.
“CCM tunaamini tumefanya kazi kubwa, kwa hiyo tutauza ilani kwa wananchi, tutawashawishi naamini watatuchagua, kwahiyo tukichaguliwa msilalamike.”
Makalla pia ametumia nafasi hiyo kuelezea mafanikio ya CCM katika kuwahamasisha wanachama na wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura, akibainisha kuwa mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa idadi ya waliojiandikisha.
“Kuna vyama vilihamasisha watu wake wasiende kujiandikisha. Nafurahi kwamba CCM ilihamasisha wanachama wake na wapenda maendeleo kwa ujumla kujitokeza, na kweli wakajitokeza kwa wingi.” Ameeleza.
Kauli hiyo imekuja wakati nchi ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo Watanzania wanatarajiwa kuwachagua viongozi wa ngazi ya urais, ubunge, udiwani na wawakilishi wa Zanzibar, huku mjadala kuhusu mazingira ya uchaguzi ukiendelea kushika kasi miongoni mwa wadau mbalimbali wa kisiasa na kijamii.