Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Hassan Mtenga, amekabidhi mifuko ya saruji 100 kwa kata zote 18 za Manispaa ya Mtwara Mikindani. Saruji hiyo imetolewa kama sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake ya kusaidia juhudi za Chama cha Mapinduzi (CCM) katika ujenzi wa ofisi za chama kwenye kata hizo.
Akikabidhi msaada huo, Mtenga amewahimiza viongozi wa chama kuhakikisha saruji hiyo inatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa ili kufanikisha ujenzi wa ofisi hizo na kuimarisha shughuli za chama ngazi ya kata.
Diwani wa Kata ya Jangwani, Juma Salumu, ameishukuru msaada huo huku akieleza changamoto wanazokabiliana nazo kwa sasa. Amesema, “Hivi sasa tunafanya vikao vya ndani kwenye vibanda vya kuonyesha video (vibanda umiza), hali ambayo inahatarisha usalama wa siri za chama. Kupitia msaada huu, tutahakikisha tunasimamia vyema ujenzi wa ofisi.”
Katibu wa CCM wa Kata ya Ufuko, Hamisi Ally, naye amepongeza juhudi za Mbunge Mtenga na kuomba msaada zaidi wa kokoto na mchanga ili kukamilisha ujenzi wa ofisi hizo. Ameeleza kuwa ujenzi tayari umeanza, ambapo vyumba viwili vya ofisi vimeinuliwa pamoja na choo.
Mtenga Apata Sifa za Viongozi wa Mitaa
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mnazi Mmoja, Kata ya Mitengo, Issa Mpondomoka, amempongeza Mtenga kwa kujali maendeleo ya chama. “Wabunge wengi wamepita, lakini hawakufanikisha ujenzi wa ofisi za chama. Tunashukuru kwamba Mtenga ameonesha kujali msingi wa chama unaoanzia matawi na kata,” alisema.