Latest Posts

MIAKA 50 YA MAFUNZO YA UFUNDI STADI: VETA YAJIVUNIA MAFANIKIO MAKUBWA

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeeleza mafanikio makubwa iliyoyapata tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994, ikiwemo ongezeko la vyuo vya ufundi stadi kutoka 14 hadi 80, kuongezeka kwa vyuo binafsi hadi zaidi ya 770, na kupanuka kwa wigo wa udahili wa wanafunzi kutoka 38,560 hadi 380,000 kwa mwaka.

Akizungumza siku ya Ijumaa Februari 21, 2025 mkoani Singida katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa kanda zote nchini, sambamba na kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa VETA, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, CPA Anthony Kasore, amesema ongezeko la vyuo na wanafunzi ni mafanikio makubwa yanayoonesha dhamira ya serikali katika kuwezesha vijana kupata ujuzi wa kiufundi unaohitajika sokoni.

“Tangu VETA ianzishwe, tumeona mabadiliko makubwa. Mwaka 1994, vyuo vya VETA vilikuwa 14 pekee, lakini leo tuna vyuo 80 vilivyopo katika wilaya na mikoa mbalimbali nchini. Pia, sekta binafsi imeonesha ushirikiano mkubwa ambapo idadi ya vyuo binafsi imeongezeka kutoka chini ya 50 hadi zaidi ya 770, hivyo kufanya jumla ya vyuo vya ufundi stadi nchini kufikia zaidi ya 870,” amesema CPA Kasore.

 

Ameongeza kuwa ongezeko hilo la vyuo limechangia kupanuka kwa wigo wa udahili wa wanafunzi, ambapo mwaka 1994 vyuo vilivyokuwepo vilikuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 38,560 kwa mwaka, lakini leo hii, vyuo vyote vya ufundi nchini vina uwezo wa kudahili zaidi ya wanafunzi 380,000 kwa mwaka.

“Katika vyuo vya VETA pekee, mwaka 1994 tulikuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,940, lakini leo tunadahili zaidi ya 83,900. Ongezeko hili linaonesha jinsi elimu ya ufundi inavyopewa kipaumbele na serikali ili kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi,” amesisitiza CPA Kasore.

Serikali pia imewekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya elimu ya ufundi, ambapo tangu kuanzishwa kwa VETA, imewekeza shilingi bilioni 516 katika ujenzi wa vyuo hivyo. Awali, ilianza na uwekezaji wa shilingi bilioni 116 pekee katika vyuo 14 vya kwanza, lakini kufikia sasa, kiasi hicho kimeongezeka maradufu ili kusaidia kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi.

CPA Kasore amesema kuwa kwa sasa serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vingine 65 kote nchini, ambavyo vitasaidia kuongeza idadi ya wataalamu wa ufundi nchini.

“Serikali imeshatenga na kutoa shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivi vipya. Kati ya hivyo, kimoja kitakuwa cha Mkoa wa Songwe, huku vingine 64 vikijengwa katika wilaya mbalimbali nchini. Tunatarajia mwishoni mwa mwaka huu idadi ya vyuo vya VETA itafikia 145,” amesema.

Katika kuadhimisha mafanikio hayo, VETA inafanya maadhimisho ya miaka 50 ya utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi nchini, sambamba na kusherehekea miaka 30 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo rasmi mwaka 1994.

CPA Kasore amesema kuwa maadhimisho hayo yataambatana na shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo wanafunzi wa VETA kutoa huduma za kiufundi kwa taasisi za umma. Miongoni mwa majengo yatakayonufaika na huduma hizo ni jengo la utawala la Manispaa ya Singida, lililopo mtaa wa Karakana, ambapo wanafunzi wa VETA watafanya matengenezo na kuweka mfumo wa umeme.

Kwa ngazi ya kitaifa, maadhimisho hayo yatazinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam mnamo Machi 18 na kufungwa Machi 21, 2025, huku kwa Kanda ya Kati, shughuli hizo zikitarajiwa kuanza rasmi Februari 25 na kuhitimishwa Februari 27, 2025.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!