Na Josea Sinkala, Sinkala.
Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Lupa Yohana Mpamba (Mcotton), amesema anamuunga mkono Mbunge wa jimbo la Kawe askofu Dkt. Josephat Gwajima (CCM) juu ya tatizo la utekaji nchini na kuhoji Serikali kuendelea kunyamaza kimya badala ya kukemea na kukomesha matukio hayo.
Kiongozi huyo mtendaji wa CHADEMA wilayani Chunya, amesema hayo wakati wa mazungumzo yake maalumu na Jambo Tv wilayani humo (Chunya).
Mpamba (Mcotton) ameeleza kusikitishwa na matamko mbalimbali ya baadhi ya wabunge walioinuka kumjibu kwa kejeli Mbunge na askofu Josephat Gwajima huku akisema wameshindwa kujibu hoja za utekaji na Serikali kushindwa kudhibiti matukio ya utekaji badala yake wamekuwa wakieleza kuchukizwa na hoja za askofu Gwajima.
Amesema hoja za askofu Gwajima ni sawa na zile zinazopiganiwa na CHADEMA chini ya mwenyekiti wake wa Taifa Tundu Lissu na kutaka uwajibikaji akisema wizara ya mambo ya ndani ya nchi chini ya Waziri wake Mhe. Innocent Bashungwa imekaa kimya huku wananchi wake wakiendelea kutekwa na kupotea katika mazingira ya utata.
Hata hivyo ameishauri Serikali kuingilia kati kukomesha matukio ya utekaji nchini akidai hata bunge limeshindwa kusimama kwenye eneo lake kujadili hoja hiyo na kuiagiza Serikali badala yake wabunge wengi wamekuwa wapambe wa vyama wakati Taifa lina matukio mbalimbali ambayo sio mazuri.