Na Amani Hamisi Mjege.
Mkutano wa kwanza wa Uwekezaji wa Nishati Tanzania (Tanzania Energy Investment Summit) unatarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza tarehe 12 hadi 13 Novemba 2024, jijini Dar es Salaam.
Tukio hili limepangwa kuwaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya nishati kutoka ndani na nje ya nchi, huku likiungwa mkono na washirika muhimu kutoka sekta za binafsi na serikali. Lengo kuu la mkutano huu ni kutoa jukwaa la kipekee la majadiliano, kushirikiana maarifa, na kubadilishana mawazo kuhusu mustakabali wa uwekezaji wa nishati nchini Tanzania.
Mkutano huo ulioandaliwa kwa ushirikiano wa HBZ International na Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (TAOMAC- Tanzania Association of Oil Marketing Companies) unalenga kuendana na juhudi za Tanzania za kuwa kitovu cha nishati safi na maendeleo endelevu ya sekta hiyo.
Tukio hili pia limepata uungwaji mkono kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) pamoja na taasisi nyingine muhimu za serikali zinazohusika na usimamizi wa nishati.
Kwa mujibu wa waandaaji, mkutano huu utakuwa ni tukio muhimu katika mabadiliko ya kiuchumi yanayofanyika nchini Tanzania, hasa katika sekta ya nishati. Akizungumza kuhusu umuhimu wa mkutano huo, Mkurugenzi wa HBZ International, Bw. Herman Zaidin alisema “Huu ni wakati muafaka kwa Tanzania kuandaa mkutano kama huu, kwani nchi inaendelea kujijenga kama kitovu muhimu cha nishati na soko linalojitegemea la nishati duniani. Tunawakaribisha wadau wote wa sekta ya nishati kushiriki nasi kwenye tukio hili muhimu.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Camel Oil (sehemu ya Amsons Group) na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TAOMAC, Bwana Salim Baabde, amesisitiza kuwa mkutano huu umeandaliwa kwa wakati muafaka, akisema kuwa “Muda wa tukio hili hauwezi kuwa bora zaidi.”
Baabde amefafanua kuwa serikali ya Awamu ya Sita ya Tanzania imeanza kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa Kupika kwa Nishati Safi (2024-2034), ambao lengo lake ni kuhakikisha kwamba asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi kwa ajili ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Aidha, Tanzania imekuwa ikishuhudia maendeleo makubwa katika miradi mikubwa ya nishati, ikiwemo kuzinduliwa kwa Mradi wa Julius Nyerere wa Umeme wa Maji, wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TAOMAC, Bw. Raphael Mgaya, amesisitiza kuwa tukio hili litakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa nishati.
“Ni heshima yetu kuandaa tukio hili kubwa la kipekee. Tunaamini litakuwa jukwaa zuri kwa wadau wa nishati kukutana na kushirikiana na watunga sera, wafadhili, wasimamizi, wasambazaji, na wawekezaji. Washiriki wataweza kuelewa mazingira ya kisheria na sera yaliyopo Tanzania na vilevile kujifunza kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya nishati. Wanachama wetu na wasambazaji wengine watapata nafasi ya kuonesha bidhaa na huduma zao kwa washiriki, hivyo kuboresha bishara zao”, amesema Bw. Mgaya.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na waandaaji wa mkutano, tukio hili la kipekee linatarajiwa kuvutia wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo watunga sera, wawekezaji, wasambazaji, na viongozi wa sekta ya nishati.
Mkutano huu utatoa fursa kwa washiriki kupata uelewa wa kina kuhusu hali ya sasa ya sekta ya nishati nchini Tanzania, huku wakijadili fursa mpya za uwekezaji na changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Pia, mkutano utaangazia masuala muhimu kama uwekezaji katika nishati safi, maendeleo ya miradi, pamoja na kubadilishana mawazo kuhusu suluhisho la changamoto za nishati zinazokumba sekta hiyo.
Tanzania Energy Investment Summit ina dhamira ya kutoa jukwaa ambalo litachangia kuleta uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati nchini, sambamba na kufungua milango kwa maendeleo endelevu ya nishati safi.
Huu ni mkutano wa kipekee ambao una lengo la kujenga Tanzania kama taifa lenye nguvu katika sekta ya nishati, na kuwa mchezaji mkuu katika soko la kimataifa la nishati.
Kuhusu Waandaaji
HBZ International, ni shirika la kimataifa la mawasiliano lenye zaidi ya miaka 10 ya uzoefu na miradi zaidi ya 300 iliyokamilishwa duniani kote. HBZ imeungana na TAOMAC, mdaui mkuu katika sekta ya nishati ya Tanzania, na wadau wengine wakubwa katika sekta hiyo ya nishati kuleta kuandaa kongamano hili muhimu.
Ili kujifunza zaidi kuhusu Kongamano la Uwekezaji wa Nishati Tanzania na kujisajili ili kushiriki, tafadhali tembelea https://teis2024.com.