Mkuu wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Bi. Dina Mathamani, ametoa wito kwa maafisa utumishi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanawajibika ipasavyo wanapotekeleza majukumu yao kwa wananchi, hususan kwa kuibua changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.
Akizungumza katika mafunzo ya elimu ya uraia na utawala bora yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Bi. Mathamani amesisitiza umuhimu wa kuzingatia misingi ya utawala bora ili kuwezesha wananchi kufahamu na kufanikisha mahitaji yao.
Mafunzo hayo, yanayoratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria, yamelenga kuwaongezea weledi viongozi wa serikali katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya sheria na utawala bora. Bw. Hamis Mjanja, mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), alisema kuwa mafunzo hayo yamekusudia kukumbusha viongozi umuhimu wa kuzingatia uwajibikaji katika nafasi zao za uongozi.
“Ni jukumu la kila kiongozi kuzingatia utawala bora katika utendaji wa kazi zao. Hii itasaidia kuimarisha mahusiano kati ya serikali na wananchi,” alisema Bw. Mjanja.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, wakiwemo Hedetrides na Frank Michael, watendaji wa kata, walieleza kuwa elimu waliyopata itasaidia kuboresha utendaji wao. Waliahidi kuzingatia misingi ya sheria na utawala bora katika kuwahudumia wananchi.
Mafunzo haya yameshafanyika katika mikoa mitano na kwa sasa yanaendelea katika mikoa sita, ikiwemo Kigoma, Kilimanjaro, Geita, Katavi, Tabora, na Mtwara. Lengo ni kufikia jumla ya mikoa kumi na moja, na kukamilika kwake kutaimarisha uwajibikaji wa viongozi wa serikali katika ngazi mbalimbali.